Header ads

Header ads
» » JK KUTEUA BARAZA JIPYA LA MAWAZIRI



KWA UFUPI Mara nyingi katika uteuzi wake Rais Kikwete amekuwa na utaratibu wa kuwapandisha baadhi ya naibu mawaziri kuwa mawaziri, kuwapa uwaziri wabunge ambao amewateua au kuteua waziri kutoka katika mkoa ambao anatokea waziri aliyeondolewa.

 Dar es Salaam. Wakati wowote Rais Jakaya Kikwete anatarajia kuipanga safu mpya ya Baraza la Mawaziri kwa kuteua waziri mwingine wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi baada ya kumwondoa aliyekuwepo, Profesa Anna Tibaijuka. Mara nyingi katika uteuzi wake Rais Kikwete amekuwa na utaratibu wa kuwapandisha baadhi ya naibu mawaziri kuwa mawaziri, kuwapa uwaziri wabunge ambao amewateua au kuteua waziri kutoka katika mkoa ambao anatokea waziri aliyeondolewa. Profesa Tibaijuka ambaye ni Mbunge wa Muleba Kusini mkoani Kagera anakuwa waziri wa tatu kutoka mkoa wa Kagera kuondolewa madarakani katika uwatala wa Rais Kikwete. Ameondolewa kutokana na kukabiliwa na kashfa ya uchotaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow. Wengine walioondolewa kutoka mkoa huo ni aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki kutokana na kushindwa kuwajibika katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi aliyeondolewa kutokana na sakata la Richmond. Iwapo Rais Kikwete atazingatia utaratibu wake wa kuteua waziri kutoka mkoa ambao waziri aliyeondoka anatoka, huenda nafasi iliyoachwa wazi na Profesa Tibaijuka kuchukuliwa na Charles Mwijage (Muleba Kaskazini), Gosbert Blandes (Karagwe). Assumpter Mshama (Nkenge), Jasson Rweikiza (Bukoba Vijijini), Eustace Katagira (Kyelwa), Deogratius Ntukamazina (Ngara) na Dk Antony Mbasa (Biharamulo Magharibi). Kama akitumia utaratibu wa kumpandisha naibu mawaziri, huenda nafasi hiyo ikachukuliwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene ambaye ni Mbunge wa Kibakwe au naibu mawaziri kutoka wizara nyingine kama alivyowahi kufanya mara nyingi. Kwa mujibu wa Ibara ya 66 (1) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kama ilivyofanyiwa marekebisho inampa mamlaka Rais kuwateua wabunge 10, mpaka sasa ameshawateua wanane na kubakiza nafasi mbili pekee. Kati ya wabunge wanane walioteuliwa na Rais Kikwete, watano walipewa wizara za kuziongoza. Wabunge hao na wizara zao kwenye mabano ni Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Profesa Makame Mbarawa (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia). Wengine ni Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini), na Saada Mkuya (Nishati na Madini) na Janet Mbene (Naibu Waziri Viwanda na Biashara) na Dk Asha-Rose Migiro. Dk Migiro aliteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Wabunge ambao wameteuliwa na Rais, lakini hakuwapa uwaziri mpaka sasa ni Zakia Meghji na James Mbati

Waliowahi kupandishwa
Pia Rais Kikwete amekuwa na utaratibu wa kuwapandisha baadhi ya manaibu waziri kuwa mawaziri.
Amefanya hivyo kwa Dk Nchimbi ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani alikuwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana na Michezo. Awali alikuwa  Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Mwingine ni aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, ambaye kabla ya kushika nafasi hiyo alikuwa naibu waziri wa wizara hiyo wakati huo ikiongozwa na Shamsa Mwangunga.
Kagasheki pia alipandishwa kutoka naibu waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi hadi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.
Rais Kikwete alipoingia madarakani alimpandisha aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji na Mifugo wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Anthony Diallo kuwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo.
Mwingine aliyepandishwa ni William Ngeleja, ambaye aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, baadaye alipandishwa kuwa waziri kamili katika wizara hiyo.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe aliteuliwa katika nafasi hiyo baada ya kuitumikia nafasi ya naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi.
Naye aliyewahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami, aliteuliwa na Rais Kikwete kushika wadhifa huo baada ya kuwa Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko.
Celina Kombani aliteuliwa kuwa Naibu Waziri Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), baadaye alipandishwa na kupewa Wizara ya Katiba na Sheria. Hivi sasa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi), ofisi aliyopewa kuiongoza tangu mwaka 2012.
Kwa upande wake, aliyekuwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo, Dk Mathayo, kabla ya kupewa nafasi hiyo alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
Mawaziri waliohimili mitikisiko
Pamoja na kuwapo kwa panga pangua ndani ya baraza la mawaziri, wapo baadhi yao ambao wamefanikiwa kudumu katika baraza hilo tangu Rais Kikwete aingie madarakani ambao ni Sofia Simba, Profesa Mark Mwandosya, Stephen Wassira, Dk Hussein Mwinyi na Dk John Magufuli. Wengine ni  Profesa  Jumanne Maghembe, Dk Shukuru Kawambwa, Hawa Ghasia na Dk Mary Nagu.
Kauli ya wasomi
Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Faraja Christoms, alisema; “Tatizo ni mfumo. Serikali ya awamu ya nne imekuwa na udhaifu katika mfumo wake wa kufuatilia utendaji kazi wa watumishi wa Serikali. Rais Kikwete alipoingia madarakani alitembelea kila wizara na kusisitiza uwajibikaji, ila sidhani kama amekuwa akifuatilia wizara zinatenda yapi.”
Aliongeza, “Nadhani hata watendaji wa Serikali wameshajua kuwa Rais siyo mfuatiliaji nao wanafanya mambo watakavyo.”
Alisema jambo kubwa linaloitafuna nchi ni vigogo wa Serikali kufanya kazi kwa kulindana, kukosekana kwa dhamira ya uwajibikaji na kupeana nafasi za kazi kwa kujuana na akisisitiza kuwa mtumishi bora ni yule mwenye uwezo na dhamira ya kufanya kazi.
Profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chris Maina alisema; “Ili kupata kiongozi mzuri ni lazima anayemteua au kumpendekeza awe na uhakika kuwa mtu hisika ni mwadilifu, hicho ndiyo kigezo kikubwa. Pili, lazima mtu huyo awe mtendaji na utamjua kwa kutazama kazi alizozifanya awali, yaani historia yake katika utendaji.”  Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema, “Tatizo ni mfumo. Hatuna mfumo unaowandaa watu kimaadili, hilo limesababisha hata jamii nzima kukosa maadili ambayo ndiko wanakotoka hao mawaziri na viongozi wengine.”

Alisema hata vyombo vya kusimamia uwajibikaji, rushwa na maadili ni dhaifu. “Vyombo hivi havina meno na unaweza kudhani kuwa vipo kwa ajili ya kuwalinda watu fulani fulani tu. Nchi za Ulaya huwezi kukuta yanatokea mambo kama ya hapa kwetu kwa sababu wana vyombo vinavyofuatilia watendaji kwa ukaribu zaidi na kuwachukulia hatua wanaokiuka maadili,” alisema Profesa Makulilo.

Imehaririwa na;- poatel Africa

Habari yako! Endelea kutembelea Tovuti ya TeknoTaarifa kwa Taarifa murwa za Teknolojia kutoka ndani na nje ya Tanzania, Tupo kwa ajili ya wapenzi wa Teknolojia.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post