Header ads

Header ads
» » IKULU:: RAIS HAJAWADHALILISHA WABUNGE


KURUGENZI ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, imesema habari zilizochapishwa katika gazeti la Tanzania Daima linalomilikiwa na chama cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) la jana, limeandika habari kwenye ukusara wake wa mbele chini ya kichwa cha habari: “Wabunge: Ikulu imetudhalilisha” hata kama wabunge wanaokaririwa katika habari hiyo ni wawili tu, Freeman Mbowe na David Kafulila.

Habari hiyo inadai kuwa, Ikulu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kwa kuteua Mwenyekiti wa Bodi Mpya ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kwa ‘kumruhusu’ Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo kuteua wajumbe wapya wa bodi hiyo, wamewadhalilisha wabunge na “kuwafanya waonekana wajinga kwa sababu maamizio yao yametupwa.”

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, imetoa ufafanuzi kuhusu madai hayo ya Mbowe na Kafulila:

Ilisema kuwa, Rais Kikwete, kamwe hajapata kulidhalilisha Bunge ama Wabunge. Anafurahishwa na kazi yao nzuri na ushirikiano wao kwa Serikali yake. Rais Kikwete alirejea kusisitiza jambo hili juzi tu na kulipongeza Bunge kwa kazi nzuri katika Salamu za Mwaka Mpya kwa Wananchi, Alhamisi iliyopita usiku.

Kurugenzi hiyo ilisema Kwamba, uteuzi wa Mwenyekiti Mpya wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco, Profesa Mighanda Manyahi, uliofanywa na Rais wiki iliyopita, unatokana na mamlaka aliyonayo kisheria na wala haukulenga kumdhalilisha yoyote, kama ambavyo teuzi nyingine nyingi azifanyazo, hazilenga kumfanya mtu yoyote “mjinga”.

Pia, ilisema hadhi ya sasa ya Profesa Muhongo, kama Waziri wa Nishati na Madini, bado inampa madaraka ya uteuzi kwa bodi zilizoko chini ya Wizara yake na wala hajapoteza “sifa ya kuendelea kuwa ofisini na hivyo kukosa sifa ya kuteua Wajumbe wa Wakurugenzi wa Tanesco” kama wanavyodai wabunge hao wawili.

Ilisema kwamba, uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco na wajumbe wa bodi hiyo ni ushahidi mwingine usiopingika wa utekelezaji thabiti wa Maamizio ya Bunge lililojadili suala zima la Akaunti ya Escrow ya Tegeta na ushauri wa Bunge hilo kwa rais kumshtumu kwa hatua yake ya kutekeleza ushauri wa Bunge ni jambo la kushangaza sana.

Kwamba, tofauti na baadhi ya shutuma za wabunge wa upinzani, Rais ametekeleza kikamilifu kabisa ushauri uliotolewa kwake na Bunge katika maamizio yote nane, moja baada ya nyingine, ukiwemo ushauri kuhusu Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco na kuwajibishwa kwa maofisa mbalimbali wa umma na waandamizi wa Serikali.

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, inapenda kuwashauri Mbowe na Kafulila wakubali kufuata misingi ya haki ya kibinadamu katika kushughulika na watu wengine.

Imehaririwa na;- poatel Africa

Habari yako! Endelea kutembelea Tovuti ya TeknoTaarifa kwa Taarifa murwa za Teknolojia kutoka ndani na nje ya Tanzania, Tupo kwa ajili ya wapenzi wa Teknolojia.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post