Header ads

Header ads
» » UHABA WA MADARASA TATIZO KUBWA MKOANI GEITA

 
Wanafunzi wa darasa la pili katika shule ya msingi Nyamarere mkoani Geita wakiwa darasani. 

Geita. Tunaweza kusema ni majanga ya elimu. Tunasema hivi maana ni kama hakuna lugha rahisi ya kuelezea hiki kinachoonekana katika shule mbili za msingi; Nyamarere na Bweya zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita au Geita Vijijini kama ambavyo wengi hupenda kutamka.
Wanafunzi katika shule zote mbili wanaishi katika mazingira ya enzi za ujima kwani wengi wao wanasomea nje kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa na baadhi yao chini ya miti ili kusaka kivuli, wakati wale wanaopata fursa ya kuingia katika madarasa wanakalia mawe kutokana na ukosefu wa maadawati.
Kuna nyakati ambazo wanafunzi wa madarasa mawili au matatu wanalazimika kutumia chumba kimoja na hapo mwalimu akiingia, huwafundisha walio wake kwa maana ya darasa husika na wale wa madarasa mengine huwa watazamaji iwe kwa dakika arobaini au themanini za somo.
Shule ya Msingi Nyamarere yenye madarasa ya kwanza mpaka sita, ina wanafunzi 742; wasichana 315 na wavulana 427 pamoja na walimu 12. Shule hii ina madarasa mawili tu na ofisi moja ya mwalimu mkuu ambayo pia hutumika kama maktaba na stoo.
Hii inamaanisha kuwa kwa idadi ya wanafunzi waliopo, chumba kimoja cha darasa kinapaswa kukaliwana wastani wa wanafunzi 371. Kwa upande wake, Shule ya Msingi Bweya yenye wanafunzi 401 ina vyumba vitatu, hivyo wastani wa wanafunzi katika darasa moja ni 134.
Niliwasili katika Shule ya Nyamarere muda wa saa 04:00 asubuhi na ilikuwa ni asubuhi tulivu huku anga likiwa limefunikwa na mawingu yaliyoashiria kwamba huenda mvua ingenyesha siku hiyo.
Nilipokewa vyema na mwanafunzi aliyejitambulisha kwa jina la Neema Martine ambaye alinikimbilia baada ya kuniona.
Mwanafunzi huyo aliyeonyesha nidhamu ya hali ya juu, aliniamkia kisha kunipokea mizigo yangu akiamini pengine kuwa mimi ni mwalimu mpya.
Baada ya kusalimiana, Neema aliwaongoza wanafunzi wenzake waliokuwa wameketi katika moja ya makundi mengi yaliyokuwa katika eneo hilo la shule akisema: “Heshima kwa mwalimu toa.”
Wanafunzi walisimama na kupiga saluti wakisema kwa pamoja: “Shikamaoo mwalimu”. Baada ya tukio hili waliketi na kuendelea na kile ambacho walikuwa wakifanya, ambacho kwa wakati huo sikufahamu kilikuwa ni kitu gani.
Kadiri nilivyokuwa nikiingia katika mazingira ya shule hii ya Nyamarere nilianza kuhisi kwamba makundi kadhaa ya wanafunzi niliowaona wakiwa wameketi nje, ni madarasa na walimu wao walikuwa wakiendelea kufundisha.
Wapo waliokuwa wameketi sehemu za wazi, wengine pembezoni mwa kuta za vyumba vya madarasa vilivyopo, wengine waliketi chini ya miti mikubwa ya miembe na wengine walikuwa wakiendelea na masomo katika boma la jengo ambalo halijaezekwa.

Imehaririwa na;- poatel Africa

Habari yako! Endelea kutembelea Tovuti ya TeknoTaarifa kwa Taarifa murwa za Teknolojia kutoka ndani na nje ya Tanzania, Tupo kwa ajili ya wapenzi wa Teknolojia.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post