New Delhi. Mfanyabiashara Leonard Willoughby aliwahi kusema;
‘siku utakayoanza kuishi kwa kuifuata mipango yako unayopanga, kila kitu
katika maisha yako kitabadilika kabisa.’ Inawezekana watu wengi
wanaufahamu msemo huo, lakini Ramesh Babu anajitapa kuyatendea kazi
maneno hayo.
Babu ambaye ni kinyozi bilionea pekee nchini
India, anasema aliuchukua ushauri wa Willoughby na kuamua kuutendea kazi
tangu siku ya kwanza alipousikia na kwamba maisha yake yalianza
kubadilika.
Kwa mujibu wa Jarida la ‘Your story’ la nchini
India, Babu amefanikiwa kuvuka vizingiti kadhaa vya umaskini hadi
kufikia kuwa mmoja wa watu maarufu nchini humo akiwa na uwezo wa kununua
gari aina yoyote anayoitaka.
Asema kuwa mwaka 1994 alinunua gari lake la kwanza
aina ya Maruti, lakini aliendelea na kuhifadhi fedha kidogo kidogo
alizokuwa anazipata hadi mwaka 2004, alipoanzisha kampuni ya kokodisha
magari, ikiwa na magari saba wakati huo.
Hadi kufikia mwaka huu, kinyozi huyo amelinunua
magari 75 kati ya hayo matano ni ya kifahari yakiwemo, Mercedes, BMW,
Audi, mabasi kumi na lile analolipenda liitwalo Rollsw Royce.
Pamoja na utajiri huo mkubwa alionao Babu, bado
anaendelea na kazi yake ya kinyozi. Akisimulia maisha yake ya awali,
anasema kuwa alizaliwa katika familia masikini, baba yake alikuwa
kinyozi na kwamba alifariki mwaka 1979 wakati Babu akiwa na miaka saba.
“Baba yangu alituachia biashara ya saluni Mtaa wa
Brigade ambalo mjomba wangu alichukua akaanza kuiongoza. Anawa anatupa
kiasi kidogo cha fedha. Tulikuwa tunakula chakula kimoja kwa siku ili
tuweze kuishi tu,” anasimulia.
Anasema alipokuwa shule ya msingi, alilazimika kufanya kazi ili kuweza kujikimu kimaisha kwa kupata kiasi kidogo cha fedha.
“Nilikuwa nikibeba magazeti na chupa za maziwa na
kitu kingine chochote ambacho kingeweza kupunguza ugumu wa maisha ya
mama yangu. Hii ndiyo sababu ya kuhitimu masomo yangu,” anasema.
Baadaye alifanikiwa uendelea na masomo yake, jambo
lililomfanya mama yake aanzishe ugomvi na mjomba aliyekuwa akisimamia
duka baada ya kugoma kutoa fedha za matumizi.
“Ndipo nilipomwambia mama nitachukua saluni na
kukiendesha mwenyewe. Hakupenda uamuzi huo kwa kuwa alifikiri nitaacha
masomo, lakini nilianza kazi hiyo.
“Asubuhi nilikuwa saluni, jioni nilikwenda
masomoni kisha usiku nilikuwa saluni tena na kufanya kazi hadi saa 7
usiku. Hivyo ndivyo nilivyoanza kuitwa kinyozi,” anasema.