Huduma zote za intaneti kwenye simu za mkononi zimeendelea kuzimwa nchini Ethiopia kwa siku saba sasa, wakati matukio ya ghasia za maandamano yakiendelea sambamba na “hali ya hatari” iliyotangazwa hivi karibuni.
Maandamano yamekuwa yakifanyika mara kwa mara kwenye majimbo ya Oromia tangu Novemba 2015, kufuatia madai ya kutaka kujitawala, kupata uhuru na kuheshimiwa kwa watu wa kabila la Oromo, ambao wamekuwa wakidaiwa kubaguliwa na kuteswa na mfumo wa serikali kwa zaidi ya robo karne iliyopita. Vyombo vya dola vimetumia nguvu kupita kiasi katika kujaribu kupambana na waandamanaji kwa zaidi ya tukio moja. Mnamo Oktoba 2 pekee, watu 52 waliuawa. Chama cha upinzani cha Oromo Federalist Congress (OFC), kimeripoti idadi ya vifo vinavyofikia watu 600.
Wakati baadhi ya mitandao ya kijamii ikifungwa kama vile WhatsApp kadri maandamano yanavyoendelea kushika kasi, jijini Addis Ababa, ambao ni mji mkuu, hili ndilo tukio refu zaidi ya kuzimwa kwa huduma za mtandao wa Intaneti kuwahi kutokea nchini humo.
Kunyamazishwa ghafla kwa waandamanaji kwenye mitandao ya kijamii kumewafanywa wale wanaofuatilia habari za maandamano hayo kwenye mtandao wa Facebook na Twitter kupatwa na wasiwasi.
Kuzimwa kwa intenti ya simu za mkononi kunaweza kusababisha kupungua kwa habari zinazohusu maandamano hayo kwenye mitandaoani. Wanaharakati wanawasi kuwa maandamano hayo, ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakitegemea mitandao ya kijamii katika uratibu wake na kusambaza ujumbe kwenda kwa wafuatiliaji wa kimataifa, yataathirika sana kwa kukosekana kwa njia kuu ya mawasiliano. Ingawa si maeneo mengi yameunganishwa na mtandao wa intaneti, mitandao ya kijamii imekuwa muhimu sana -hasa kwa ajili ya maandamano yanayofanyika kwenye majimbo ya Oromia na Amhara. Habari zinazopatikana kwenye kurasa za Facebook na Twita hazioneshi kuwepo kwa machapisho mengi kama ilivyokuwa juma lililopita.
Chanzo: africanews.com