NI wazi kuwa sasa hivi ni rahisi kwa mtu kutumia simu yake ya kiganjani, tablet au hata laptop kutafuta na kupata taarifa zote kuhusu klabu anayoipenda duniani.
Ndiyo, hapo ndipo teknolojia ilipotufikisha, ukiachilia mbali tu ile inayotumika viwanjani kuchukua picha na kuzileta kwenye televisheni yako, lakini bado ipo hiyo inayokuwezesha kupata mikakati na mipango ya klabu.
Hili ni jambo la kujivunia kuona kuwa kila siku kuna mapya yanayoboreshwa na teknolojia katika fani hii ya michezo duniani, ambapo kwa sasa si kitendawili tena.
Wewe na mimi tunaweza kufikiri kuwa labda teknolojia inaishia hapa kulingana na haya mazuri iliyofanya hadi sasa, lakini la-hasha!, kwani baadhi ya watendaji nguli kwenye bidhaa zinazohusu michezo wameweka wazi nia yao ya kutambulisha teknolojia itakayoruhusu wewe mtazamaji kutazama na kusikiliza kile kinachozungumzwa na kocha vyumbani wakati wa mapumziko.
Mkurugenzi wa Michezo nchini Marekani, Larry Scott, amesema wanajitahidi kufanya kila linalowezekana, ikiwamo kuwekeza kiwango kikubwa zaidi cha fedha kwa lengo la kuhakikisha kuwa mfumo huo mpya unafanikiwa.
Lengo ni kuwapa uhuru wa kusikia na kuona kinachoelezwa na kocha moja kwa moja kutoka kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Anasema nia yake ni kuona mpango huo ukianza kutekezwa mwaka huu na kwamba hadi kufikia kwenye michuano ya Kombe la Dunia mwakani uwe umeshazoeleka.
Pia jambo jingine ni kwamba, teknolojia hiyo itakuwa na uwezo wa kuonyesha makao makuu ya klabu husika kuanzia mtaa, mji, nchi na kila kitu, lengo likiwa ni kufanya mashabiki kuzifahamu zaidi timu zao au kuondoa umbali uliopo baina ya nchi wanazoishi na mazingira ya vilabu vyao wanavyovipenda duniani.
Mtendaji Mkuu wa Next VR, Brad Allen, amesema huu si wakati wa mtazamaji kuishia kumwona mchezaji wa timu anayoipenda uwanjani pekee, bali “tunahitaji kuhakikisha kuwa anafahamu mahali makao makuu ya klabu yake yalipo na vitu vyote muhimu tutamsogezea kwenye TV yake”.
Anasema kwa kuanzia, teknolojia hiyo itahusisha michezo miwili ambayo ni soka na kikapu.
“Kwa muda ambao vilabu vinakuwa mapumziko ni wakati mwafaka kwa mashabiki kuangalia maisha ya wachezaji wao na klabu kwa ujumla, natambua kuwa hilo litawezekana kwa mwaka huu kwani teknolojia inaruhusu,” anasema Allen.
Kwa teknolojia hii, ina maana kwamba tutashuhudia mambo mengi yanayohusu klabu kubwa duniani kama Barcelona, Manchester United na nyingine nyingi.