Header ads

Header ads
» » MPANGO WA ELIMU NCHINI BADO NI KIPOFU


Kuanzia juzi, tumeona makala kwa njia ya picha kuhusu hali ya kutisha na kufadhaisha iliyopo katika Shule ya Msingi ya Nyamarere, Kata ya Ikome katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, mkoani Geita. Hakika ni picha ambazo zimewafanya baadhi ya wasomaji wetu kupigwa na butwaa kwa mshangao, huku wengine wakisema picha hizo ni za kusadikika, kwa maana ya kutoamini kwamba miaka 53 baada ya Uhuru bado kuna shule za ajabu ambazo hazina hadhi wala sifa ya kuitwa shule.
Ni picha zinazoonyesha hali halisi ya mazingira ya kudhalilisha ya ufundishaji na ufundishwaji katika shule hiyo. Moja ya maajabu ya shule hiyo ni kwamba inao wanafunzi 742 kuanzia darasa la kwanza hadi la sita wanaotumia vyumba viwili tu vya madarasa, huku wengine wakiwa nje wakisomea chini ya miti. Ajabu ni kwamba mahali ilipo shule hiyo siyo mbali sana na anakoishi mbunge aliyechaguliwa na wananchi pamoja na viongozi wa ngazi za kijiji, kata, wilaya na mkoa. Viongozi hao hawajaguswa hata kidogo na matatizo yanayoikabili shule hiyo ya Nyamarere.
Ni maajabu kwa kuwa walimu wanalazimika kuwaelekeza wanafunzi kwa kuandika kwenye mchanga kutokana na madarasa kutokuwa na mbao za kuandikia. Mwandishi wetu aliwakuta walimu wakifundisha katika mazingira magumu ya kudhalilisha na kukatisha tamaa, huku wanafunzi wakiwa wamekaa ardhini, wengine juu ya mawe na wengine wakiwa wanachukua notisi huku wamechuchumaa. Shule hiyo haina madawati na walimu hawana nyumba za kuishi.
Mmoja wa walimu alikutwa akifundisha wanafunzi wa darasa la tatu namna ya kuumba herufi, lakini alikuwa akichora herufi hizo hewani kutokana na kutokuwapo ubao. Mwingine alikuwa akifundisha kwa imla kutokana na tatizo hilo, hivyo alilazimika kutamka na wanafunzi kuandika, tena wakiwa wamekaa kwenye udongo. Mwalimu aliyekuwa akifundisha hisabati darasa la pili hakuwa na ubao, hivyo kulazimika kuandika juu ya mchanga. Majina na picha za walimu wote waliokutwa katika mazingira hayo ya udhalilishaji yametokea gazetini sambamba na wanafunzi waliokuwa wakiwafundisha.
Uamuzi wa kuchapisha picha nyingi badala ya makala zenye maelezo marefu ulitokana na ukweli kwamba picha moja yaweza kutuma ujumbe mzito zaidi kuliko makala ya maneno 1,000. Picha hizo zinatoa ushuhuda usioacha shaka kwamba hiyo ndiyo hali halisi katika shule hiyo. Lakini pia pengine zitatoa fursa kwa mamlaka hizo kuchukua hatua stahiki, ingawa kuna ushahidi kwamba shule nyingi nchini zinakabiliwa na mazingira magumu zaidi kuliko yaliyopo Nyamarere.
Hali hiyo inatia shaka kama kweli Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi nchini (MMEM), siyo kiini macho. Pamoja na Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kuweka vipaumbele tisa katika sekta ya elimu, vipaumbele hivyo vimebakia tu katika makabrasha ya warasimu serikalini. Serikali haijaonyesha dhamira ya kuimarisha elimu ya msingi. Laiti ingetambua kwamba elimu ya sekondari au ya juu haiwezi kuimarika pasipo kwanza kuimarisha ya msingi, ingewekeza hapo kwanza badala ya kutumia rasilimali nyingi katika mipango mingine kama kujenga sekondari za kata au kujenga maabara katika shule hizo kwa njia za zimamoto. Ni kutokana na hali hiyo wanafunzi wanamaliza elimu ya msingi au ya sekondari bila kujua kusoma wala kuandika.

Imehaririwa na;- poatel Africa

Habari yako! Endelea kutembelea Tovuti ya TeknoTaarifa kwa Taarifa murwa za Teknolojia kutoka ndani na nje ya Tanzania, Tupo kwa ajili ya wapenzi wa Teknolojia.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post