KIPA mkongwe nchini, Juma Kaseja amelikimbia Jiji la Dar es Salaam na kuanzia msimu ujao atakuwa jijini Mbeya baada ya kukubali kusaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea Mbeya City.
Kwa miaka kadhaa, Kaseja ambaye alikuwa kipa tegemeo wa Tanzania, alikuwa katika klabu za Simba na Yanga za Dar es Salaam, mara ya mwisho akivaa jezi za njano na kijani mwaka 2014, lakini akatofautiana na wakuu wa klabu hiyo na aliyekuwa kocha Marcio Maximo.
Meneja wa kipa huyo, Athumani Tippo amezima uvumi wa habari za wapi atacheza msimu ujao, lakini zinaweza kuwa pigo kwa Kocha Mkuu wa Mwadui FC, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ ambaye alikiri katika vyombo vya habari kuwa anamhitaji mchezaji wake huyo wa zamani kikosini mwake.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kaseja alikiri kujiunga na Mbeya City na kusema anaamini bado ana uwezo wa kufanya vizuri akiwa katikati ya miamba miwili na mtaa panya.
“Kazi yangu mimi ni soka, hivyo ninahitaji kucheza ili nioneshe uwezo wangu, nashukuru Mbeya City nimemalizana nao na nitakuwa uwanjani msimu huu,” alisema Kaseja bila kutaja dau la usajili alilopewa na timu hiyo mali ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya inayofundishwa na Juma Mwambusi.
Kabla ya kusaini mkataba huo, Kaseja alikuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha msimu mmoja baada ya kuingia katika mgogoro wa kimkataba na Yanga na kumfungulia kesi kwenye Mahakama ya Kazi.
Kabla ya Yanga, Kaseja alikuwa anaichezea Simba ambayo alijiunga nayo mwaka 2002 akitokea Moro United. Aliwahi kuichezea Yanga kwa mwaka mmoja kabla ya kurejea Msimbazi.