Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Camilius Wambura alisema kuwa vijana watatu waliotoka Geita kuja jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kumuona Rais na kukaidi amri ya kusitisha safari yao, wako nje kwa dhamana.
Kauli ya Wambura inatokana na vijana watatu
kutembea kwa miguu kutoka mkoani Geita kwa lengo la kufika Ikulu kuona
na Rais na kumweleza kero zao, ambao walikamatwa baada ya kukaidi amri
ya kusitisha safari hiyo.
Wambura Alisema kinachofuata sasa ni taratibu za
kisheria ikiwamo kufanyika kwa upelelezi na ukikamilika watawasiliana na
Mwanasheria wa Serikali kufahamu hatua gani inafuata.
Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willibrod Slaa,
alithibitisha kuwa mawakili wa Chama hicho walikwenda kuwatoa vijana hao
kwa maandishi na wamechukua jukumu la kuwasimamia mahakamani iwapo
watashtakiwa.
Alisema haoni sababu ya vijana hao kukamatwa au
kushtakiwa kwa sababu walikuwa wanafanya wajibu wao, kama unampa mtu
dhamana ya kukuongoza una haki ya kuhoji endapo hakuongozi vyema na hilo
ndilo lengo la vijana hao kutaka kufikisha malalamiko yao kwa Rais.
“Wakishtakiwa mawakili wetu ambao waliwatoa jana
ndiyo watasimama mahakamani na tumewadhamini jana wameshatoka, ” alisema
Dk Slaa.
Akizungumza na gazeti hili Khalid Selemani ambaye
ndiye kiongozi wa msafara huo alisema kuwa walitolewa juzi saa moja na
nusu jioni.
Alisema chama kimeamua kuchukua jukumu la
kuhakikisha ndoto zao zinatimia kwa kufuata taratibu zote, hivyo wao
wanakisubiri chama kiwaandalie utaratibu wa kufika Ikulu.
“Tupo salama mikononi mwa Chadema ambao wamesema
jukumu hilo tuwaachie na tumekubaliana hivyo, taratibu zifuatwe ili
ikiwezekana kama tunavyoomba tuonane na Rais,” alisema Khalid.