KAMATI ya Taifa ya Matumizi Salama ya
Bioteknolojia (NBC) imeridhishwa na matumizi ya Teknolojia ya Uhandisi
Jeni (GMO) yenye lengo la kuwakwamua wakulima nchini.
Wajumbe wa kamati hiyo wakizungumza kwa
nyakati tofauti na waandishi wa habari wakati walipotembelea shamba la
majaribio la mahindi yaliyoboreshwa kwa kutumia Teknolojia ya uhandisi
jeni (GMO) chini ya mradi wa Wema katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha
Makutupora mjini Dodoma, walisema hatua iliyofikiwa na watafiti hao
ni kubwa hivyo haipaswi kuachwa ikapotea bure.
Elisa Moses kutoka Taasisi ya Chakula na
Lishe ambaye ni mjumbe wa NBC alisema teknolojia hii ya bioteknolojia
ni nzuri na inaonesha uhalisia halisi na inaweza kusaidia changamoto za
ukosefu wa chakula iliyopo nchi.
"Binafsi nimefurahi kujionea hali halisi
ya teknolojia hii hasa ninapoyaona mahindi haya ya GMO yalivyomakubwa
kwani ni muhimu sana katika kukabiliana na ukame uliopo sehemu kubwa
nchini" alisema Moses.
Meneja wa shamba hilo, Bakar Mohamed akielezea kuhusu
shamba hilo.
Mjumbe mwingine wa kamati hiyo kutoka
Chemba ya Wanyabiashara Wenye Viwanda na Kilimo, Magdalene Mkocha
alisema wamefurahi kuona jambo walilolipitisha linafanyiwa kazi vizuri
na linaleta matumaini makubwa kutokana na matokeo ya jaribio hilo.
Alisema wadau wa sekta binafsi
wanasubiri kwa hamu kuhusu matokeo hayo baada ya kuthibitishwa na
takwimu za kisayansi kwani kwa kuangalia kwa macho mahindi yanaonekana
ni bora zaidi.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Wizara ya
Kilimo Mifugo na Uvuvi Kanda ya Kati Dodoma, Sebastian Kandira alisema
hapo awali tafiti hizo zilikuwa hazifikishwi kwa wakulima ndio maana
zilikuwa hazieleweki vizuri lakini hivi sasa wameanza kuzielewa kupitia
vyombo mbalimbali vya habari.
Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo Kanda
ya Kati, Leon Mroso alisema wakati wanaanza majaribio hayo kulikuwa na
changamoto nyingi kutokana na wadau kutokuwa na uelewa hasa kwa mahindi
yaliyobadilishwa vinasaba kikubwa ni mshukuru Waziri wa Kilimo Mifugo na
Uvuvi, Charles Tizeba kwa kufika katika shamba hili la majaribio
ambalo tulipanda mahindi Oktoba 5, mwaka jana na kutupa faraja kuwa kuna
kila sababu ya kuharakisha matumizi ya teknolojia hiyo ili iweze
kutumika kama zinazofanya nchi zingine zinazofanya tafiti za namna
hiyo.