Kampeni hiyo ilizinduliwa rasmi na Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania Lazaro Nyalandu, akishirikiana na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, mashirika ya wanyama pori pamoja na msanii maarufu wa muziki nchini humo Alikiba.
Kampeni hiyo inalenga kuielimisha jamii na kuihamasisha kujiunga katika mapambano dhidi ya uwindaji haramu wa wanyama pori kama vile ndovu na wengineo.
Waziri Nyalandu alisema kuwa ndovu ni mojawapo ya vivutio vikubwa vya watalii nchini Tanzania na sekta ya utalii inachangia asilimia 17 ya mapato ya kitaifa.
Msanii wa muziki Alikiba ambaye aliteuliwa kuwa balozi wa kampeni hiyo, alidhihirisha azma yake ya kutaka kuwajibika kikamilifu kwa ajili ya kulinda wanyama pori.
Tanzania ni mojawapo ya nchi zinazotambulika kote duniani kwa mbuga zake za wanyama pori zinazovutia watalii wengi. Hata hivyo katika kipindi cha miaka 6 iliyopita., nchi hiyo imepoteza asilimia 60 ya ndovu waliowindwa kwa ajili ya biashara haramu ya pembe.