
Watu wengi wamekuwa wakila bila kufuata maadili ya afya, hivyo kuwafanya baadhi yao kuwa na afya mbaya.Picha ya Maktaba
Yanaonekana ni mambo ya kawaida, ama ni kwa mazoea au kwa kutojua lakini yana athari kubwa kwa afya na maisha kwa jumla.
Kwa siku kadhaa kuanzia leo, safu hii itaangazia
baadhi ya tabia na mienendo ya Watanzania ambayo wataalamu wanasema ni
hatari kwa maisha yetu.
Ulaji usiofaa wa vyakula
Watanzania wengi tunakosea kula kwa kutozingatia
kanuni za ulaji bora. Kwa mfano, mtaalamu wa lishe, Pazi Mwinyimvua
anasema kuwa ulaji bora ni ule unaozingatia kanuni kadhaa muhimu kama
vile kula kwa kiasi, kula vyakula vya asili, kula kwa wakati uleule kila
siku, kula mboga za majani, kuepuka kula vyakula vya kukaanga mara kwa
mara, kupunguza matumizi ya chumvi na sukari katika vyakula na kunywa
maji ya kutosha.
“ Ulaji bora pia ni pamoja na mtu kuwa na
tahadhari juu ya unywaji wa pombe, soda na juisi za viwandani, chai,
kahawa na uvutaji sigara, anasema na kuongeza kuwa ulaji wa vyakula hivi
huchangia watu kupatwa na maradhi ya Kisukari. Kuhusu unywaji wa maji,
wengi hatunywi maji kiasi kinachotakiwa kwa mujibu wa matakwa ya
kilishe. ‘’ Kunywa maji ya kutosha kuna manufaa mengi ikiwamo kuuwezesha
mwili kufanya kazi barabara, kukua vizuri, kusaga chakula vizuri,
kujikinga na maradhi, kupoza mwili, mwili kutoa sumu mwilini hasa kwa
njia ya mkojo...’’ anaongeza kutaja umuhimu wa kunywa maji.
Kwa wale wanaokunywa maji nao wanakosea kwa
kufanya hivyo punde tu baada ya kula. Wanalishe wanatueleza kuwa muda
mwafaka wa kunywa maji ni kabla ya kula au nusu saa baada ya kula
chakula.
Ama unywaji wa maji baridi ambao hupendelewa na
watu wengi, nao sio tabia ya kuiendekeza kama anavyosema Dk Samuel
Shitta: ‘’ Maji baridi kama ukinywa sana yana madhara machache kama vile
kupata vikohozi na vidonda ya koo. Pia maji baridi hasa baada ya
kumaliza kula kama wanavyofanya watu wengi kunachangia kugandisha mafuta
ya chakula ulichokula, hivyo kulifanya zoezi la usagishaji chakula kuwa
taratibu mno.
Wataalamu wanasema hali hiyo inaweza kumsababishia
mtu kukosa choo, na kuwa kama tabia itakuwa endelevu upo uwezekano wa
mnywaji baadaye kupata saratani ya utumbo, ugonjwa wa moyo na mwishowe
kifo.
Kuhusu kipimo cha matumizi ya maji kwa siku na
muda wa kunywa, mwandishi na mtaalamu wa mazoezi ya viungo, Fredy Macha
anasema mwanadamu anapaswa kunywa bilauri, glasi au vikombe nane vya
maji kila siku.
“ Maji hayo usinywe tu wakati wa kula au yote kwa
wakati mmoja, yasambazwe katikati ya siku kwa kunywa unapoamka, kabla ya
kula, nusu saa baada ya kula. Unapokunywa maji ya kutosha unalipumzisha
ini na kulisaidia kuchuja, kusafisha uchafu, takataka’’anasema.
Kula chakula kingi kupita kiasi
Aidha, wapo wanaodhani afya ni kula chakula kingi,
kama ni ugali basi uwe mkubwa mithili ya mlima. Mwili haujengwi na
wingi wa chakula kingi tena cha aina moja, bali unajengwa na ulaji wa
vyakula vya aina mbalimbali hata kama ni vichache.
Huu ndio mlo kamili maarufu Kiingereza kwa jina la Balanced
Diet. Wataalamu wa lishe wanatueleza kuwa kila mlo anaokula mwanadamu
unapaswa kuhusisha mafungu ya vyakula ambayo ni wanga, protini, vitamin,
nyuzinyuzi, madini, mafuta na maji ya kunywa.
Athari ya ulaji wa chakula kingi anaitaja
mwanalishe Pazi kwa kusema: “ Kuweka chakula kingi katika sahani
kunamfanya mtu kushindwa kudhibiti mhemko wake wa kula sana, kwa hiyo
sio ulaji bora… hivyo huchangia kwa haraka safari ya kupata maradhi ya
kisukari.’’ Aidha, upo utaratibu mbovu kwa watu wengi kupenda kula aina
moja ya chakula katika muda fulani siku zote. Kwa mfano, Watanzania
wengi wana mazoea ya kula ugali mchana na wali nyakati za usiku.
Kilishe kuna vyakula kedekede vinavyofanya kazi
sawa na ugali kama vile viazi, mihogo, ndizi na vyakula vingine jamii
ya nafaka.
Hata ulaji wa mbogamboga nao ni tatizo kwa watu
wengi. Mboga za majani zinanasibishwa na hali duni ya kipato, ni chakula
cha wasionacho. Wenye nacho wanakula nyama. Huu ni mtazamo tenge kuhusu
ulaji wa vyakula vya mbogamboga, ambavyo wataalamu wanatueleza kuwa ni
muhimu kwa uimara wa afya zetu.
Kutopenda kula ugali wa dona
Mazoea mengine ni kwa walaji wa ugali. Walaji
wengi hawataki kula unga usiokobolewa, maarufu kwa jina la dona.
Wanapenda ugali uliokobolewa ambao kimsingi hauna virutubisho vingi kama
ugali wa dona.
Japo kila aina ya unga wa ugali una faida na
hasara zake, wataalamu wengi wanashauri matumizi ya unga wa dona hata
kama unaonekana mbaya katika macho ya walio wengi.
‘’Kwa mtu anaweza kutumia unga usiokobolewa (dona)
ni muhimu kwake kufanya hivyo kwa sababu faida zake ni nyingi... unga
usiokobolewa una kiasi kikubwa cha mafuta, protini, madini, vitamini, na
nyuzinyuzi (fibre), kwa hiyo, unaimarisha zaidi lishe ya mlaji,
‘’anashauri Pazi.
Vyakula vya kufungasha
Kuna vyakula maarufu Kiingereza kwa jina la ‘Fast
Food.’ Watanzania wengi hasa vijana mijini ni waathirika wa tabia ya
ulaji wa vyakula hivi hatarishi. Vyakula hivi ni kama viazi vya kukaanga
(chips), kuku wa kukaanga, keki, pizza na biskuti.
Ukweli ni kwamba uvivu wa kupika na ulimbukeni
unawafanya vijana wengi kutonunua vyakula halisi. Wanataka vyakula vya
haraka haraka vilivyotengenezwa tayari bila ya kujali afya zao.
Madhara ya kutopenda kupika ni kuwepo kwa idadi
kubwa ya vijana, wakiwemo wanawake wasiojua kupika hata mapishi mepesi .
Ziko ndoa zinazovunjika kwa kuwa mke hajui kupika hata wali wa maji
Ulaji mwingi wa nyama
Ulaji mwingine hatari ni ule unaohusu nyama hasa
kuku wa kisasa, tabia iliyowakumba watu wengi mijini. Kimsingi wataalamu
wanasema nyama (ukiondoa ya samaki) sio nzuri kwa afya zetu.
Kwa mfano, Shirika la Kimataifa la Utafiti wa
Saratani linasema nyama zina kemikali aina ya Amino ambazo ni chanzo cha
maradhi ya saratani.
...walaji wa nyama wa kila mara wanajiweka katika
hatari ya kupatwa na ugonjwa wa saratani ya matiti na figo. Utafiti
mwingine uliofanyika Chuo Kikuu cha Harvard cha nchini Marekani,
ulibainisha ya kwamba walaji wakubwa wa nyama ya ng’ombe, kondoo, mbuzi,
na nguruwe, wako katika hatari ya kukumbwa na ugonjwa wa saratani ya
matiti hasa wanawake, ‘’anasema Esbon Kagya akinukuliwa na gazeti la
Rai la Oktoba 4 2012.
Kuna kasumba pia ya baadhi ya watu kwenda kununua
vyakula katika maduka makubwa (super market) licha ya ukweli kuwa
vyakula halisi vinapatikana katika masoko ya kawaida.
Wapo wanaofikiri kwenda katika maduka haya na
kununua bidhaa zilizofungashwa ndio usasa. Kwa Watanzania wengi bado
hatujafikia mazingira ya kununua bidhaa kama vile mboga katika maduka
ya aina hii. Kwa nini ukanunue nyanya iliyohifadhiwa mwezi mzima dukani,
wakati masoko yamesheheni nyanya kutoka shambani?
Vyakula vya mafuta
Mitaani kuna matumizi makubwa ya vyakula vyenye
mafuta mengi hasa yatokanayo na wanyama. Mafuta mengi hasa kwa vyakula
vya kukaanga kama vile chips, ni hatari kwa afya kama anavyosema
mtaalamu wa Lishe Halima Chamosi kuwa mafuta hayo yana lehemu ambayo ni
chanzo cha magonjwa mengi kama vile ugonjwa wa moyo na kibofu.
Ikibidi kutumia mafuta kama kiungo muhimu katika
vyakula , Chamosi anashauri matumizi ya mafuta yatokanayo na mimea au
nafaka kama vile pamba, alizeti, chikichi na aina nyingine ya mimea.
Uchunguzi wa afya zetu
Kilele cha kupuuzia mambo kwa Watanzania
kinajionyesha kwa jinsi tunavyodharau kupima hata hali ya afya zetu.
Jiulize wewe unayesoma makala haya umeshakwenda kupima afya yako tangu
kuanza mwaka huu unaofikia ukingoni?
Kwa kawaida wataalamu wa tiba wanasema tunapaswa
kufanya uchunguzi wa afya zetu hata kama tunafikiri hatuna maradhi
yanayotusonga. Kiwango kidogo cha upimaji wa afya ni angalau mara moja
kwa mwaka