Uchaguzi
Mkuu ujao Haupo mbali kiasi cha kufanya Watanzania wachelewe kuanza
maandalizi mapema. Ndiyo maana wengi hatushangai kuona na kusikia
wanasiasa wanaojipanga sasa kwa ajili ya uchaguzi huo.
Baadhi ya watu wanatabiri kuwa uchaguzi huo utakuwa wa kihistoria
kutokana na ushindani mkubwa wa vyama vya siasa unaozidi kushika kasi
nchini. Hata hivyo, Watanzania tunapaswa kujihadhari tusijise tukajikuta
mwaka 2015 tunamkosa rais bora kutokana na vishawishi vya kinafiki na
chuki binafsi.
Ninasema
hivyo kwa sababu viashiria vya wanasiasa wanafiki, waliojenga chuki
binafsi dhidi ya wengine na wenye uchu wa madaraka, vimeanza kuonekana
katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu. Tanzania siku hizi
imefika mahali ambapo baadhi ya wanasiasa wanaendelea kupata ujasiri wa
kutaka kuwaaminisha watu kimakosa kuwa rangi nyeupe ni nyeusi!
Fikiria, kwa mfano, wanaosema hakuna maendeleo yoyoye yaliyopatikana
nchini tangu tupate uhuru mwaka 1961. Huo ni unafiki wa dhahiri uliokuwa
ajenda kuu ya baadhi ya wanasiasa. Mfumo wa vyama vingi vya siasa
uliridhiwa nchini na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwa lengo
kuu la kuchochea mageuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, lakini yenye
tija kwa Watanzania.
Kwa
mantiki hiyo, vyama vya siasa havipo kwa ajili ya kupotosha na
kufarakanisha wananchi, ili wanafiki na wenye uchu wa madaraka wapate
mwanya wa kujineemesha na familia zao. Vyama vingi vya siasa vina faida
nyingi, ambazo ni pamoja na kusaidia kukemea na kukosoa utendaji wa
serikali iliyo madarakani inapoonekana kukiuka misingi ya uongozi bora
ulio na manufaa kwa wananchi.
Lakini
ukiona viongozi wa chama chochote cha siasa wanaelekeza nguvu kubwa
katika kupanda mbegu ya chuki na kuwagawa wananchi, ujue hao ni
wanasiasa ‘mcharuko’ wanaosukumwa na hisia za unafiki na kamwe
hawaitakii mema nchi.
Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania itajengwa na Watanzania wazalendo, wanaothamini
umoja na mshikamano chini ya misingi ya amani na upendo –
vilivyoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, na Mzee Abeid Amani
Karume.
Dhana
za ubaguzi na utengano katika jamii zilipigwa vita kwa nguvu kubwa enzi
za waasisi hao wa taifa letu. Mazingira hayo ndiyo sasa yanayowezesha
hata viongozi wa vyama vya siasa kuzunguka na kuhutubia mikutano ya
wananchi kila kona ya nchi bila kujali wanatoka wapi na wamezaliwa na
nani.
Amani
iliyojengeka nchini inaonekana kuwalewesha baadhi ya wanasiasa ambao
pengine hawajui kuwa hata wao kama si familia, ndugu, jamaa na rafiki
zao wanaweza kuathiriwa na machafuko ya kisiasa yanayoweza
kutokea. Ongezeka la unafiki miongoni mwa wanasiasa linaweza kuwa sababu
ya kumkosa kiongozi wa nchi anayetufaa ikiwa hatutakuwa makini katika
kuchambua tabia za wanaowania madaraka hayo mwaka 2015.
Elimu
ya siasa kama si ya uraia inahitajika kuwajengea Watanzania uwezo wa
kutumia vizuri haki zao za kikatiba na kidemokrasia katika Uchaguzi Mkuu
ujao; la sivyo watajikuta wamechagua rais ‘mtakavitu’. Serikali, vyama
vya siasa na asasi za kiraia vina jukumu la kuwezesha elimu hiyo.
Suala
hili ni muhimu katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu ili
kuepuka hatari ya kumpata kiongozi wa nchi kutokana na ushawishi
ulioasisiwa na hisia za unafiki, chuki binafsi na uchu wa madaraka.
Picha
halisi ya kisiasa kwa sasa inaonesha kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) vinapewa nafasi kubwa ya
kushinda kiti cha urais mwaka 2015, lakini hatuviweki kando vyama
vingine vikiwamo Civil United Front (CUF), NCCR-Mageuzi na Alliance for
Democratic Change (ADC). Yawezekana CCM na Chadema ndivyo vyenye
ushawishi mkubwa kwa Watanzania, lakini pia vyenye ushindani mkubwa wa
kisiasa nchini. Lakini tunachopaswa kuzingatia ni kutumia kigezo cha mtu
badala ya chama kuchagua rais mwaka 2015.
Gharama
za Uchaguzi Mkuu ujao ikiwezekana zielekezwe pia katika kuelimisha
wajumbe wa vikao vyenye uamuzi ndani ya vyama vya siasa, kuhusu sifa za
kiongozi bora kuwawezesha kufanya uamuzi sahihi katika uteuzi wa
wagombea urais.
Zaidi
ya hayo, Watanzania tujihadhari na wanasiasa wanafiki na wenye uchu wa
madaraka, ili tusije tukajikuta katika Uchaguzi Mkuu ujao tunajinyima
rais bora mwenye dhamira ya kuwatumikia wananchi kwa uzito unaostahili.