Watu wengi wanahangaika na biashara au kazi za kufanya baada ya kupata malipo ya uzeeni ya kustaafu. Wengi hukimbilia kuanzisha biashara mpya ambazo huwa haziwasaidii kukabiliana na maisha kwa siku zao zilizobaki.
Wengi hushindwa kufanikiwa kwa biashara wanazoanzisha kwa fedha za kustaafu. Sababu za kushindwa kwao zaweza kuwa nyingi, lakini kubwa zaidi ni uzoefu mdogo na matarajio makubwa ya mafanikio ya haraka. Ndiyo, baada ya mtu kulipwa shilingi milioni 50 au zaidi (wengi hupata chini ya hapo), mtu atanunua gari la kutembelea na kuanzisha biashara au kujenga nyumba.
Lakini kama akili yako inakuwa ni kutaka maisha mazuri, yenye kukufanya utengeneze familia yenye uwezo kifedha, basi ni lazima uwekeze akili yako katika kujiajiri badala ya kuajiriwa. Huwezi kufikia mafanikio ya kuwa tajiri kwa kufanya kazi ya kuajiriwa, labda kama utakuwa mwizi, kitu ambacho sitaki kukufundisha.
Na kujiajiri ninakozungumzia, siyo lazima kuwa na biashara kubwa kama hizi tunazoziona za hawa mabilionea tulionao. Kwa kawaida, mtu mwenye mafanikio huanza taratibu kwa mtaji au mradi mdogo, kama tunavyosikia simulizi nyingi zinazowahusu matajiri wakubwa hapa nchini, kama Said Salim Bakhresa (pichani) au Reginald Mengi.
Tunaambiwa mmoja alianza kama mwajiriwa aliyeamua kujiajiri na mwingine alianza na biashara ndogondogo kabla ya kuja kumiliki biashara kubwa na hivyo kuwa miongoni mwa watu wanaotajwa kuwa matajiri wakubwa barani Afrika.
Sasa tunapozungumza kuhusu kujiajiri, neno zuri hapa likiwa ni ujasiriamali, lazima tuzingatie kanuni zake, ambazo ni utashi wako binafsi katika mradi unaoufanya, malengo yanayofikika utakayojiwekea na kuwa tayari kukabiliana na changamoto unazozijua na usizozijua.
Kuanza harakati za kujiajiri mapema zinakufanya kuwa mtu mwenye uzoefu katika biashara, kiasi kwamba utakuwa mkomavu kuweza kubaini matapeli au hata wizi wa aina mbalimbali kwa sababu watu wabaya, huwafuata sana watu wenye fedha kwa ajili ya kuwatapeli.
Mtu anayefanya biashara kwa malengo makubwa ya muda mrefu hahitaji faida ya harakaharaka, bali kitu cha muhimu kwake ni kujenga misingi na uwekezaji wa kutosha ili kuweza kusapoti mradi. Wanaofanya biashara kwa ajili ya kupata faida ya haraka mara nyingi hawafanikiwi.
Zipo biashara nyingi unazoweza kufanya na ambazo hazihitaji mtaji mkubwa, lakini kama utakwenda nazo taratibu zitakufikisha sehemu na kuweza kufanya kitu kinachoonekana ambacho nacho kitazidi kukua kadiri muda na umakini wako unavyoendelea.Kitu cha msingi sana ambacho nimekuwa nikisisitiza kila mara ni kwamba ili uweze kufanikiwa katika ujasiriamali wako, ni lazima ujue wapi unakotaka kwenda, kwa sababu kama hujui, ni vigumu sana kufika safari unayokusudia.
Watu wengi huanzisha biashara, lakini huishia njiani kwa sababu hawajui wanachokitaka, wanaingiza hela na kuitumia bila kujali kama wanapata faida au la. Dereva mwenye akili, huliwasha gari na kuondoka kuelekea alikodhamiria na si vinginevyo.
UNGANA NAMI FACEBOOK HAPA