Wengi kwa sababu mbalimbai tumewahi kudondosha simu kwenye maji. Kwa watumiaji wa simu kudondosha simu ni suala la kawaida.
Kwa wengi baada ya kitendo hiki huwa tunajaribu kutafuta njia mbalimbali za kuokoa simu zetu ili zisiharibike zaidi.
Kwa hali ilivyo inawezekana simu kama kifaa isiwe
tatizo pale inapodondoka, lakini muhimu ni zile taarifa zilizomo ndani
ya simu.
Kuna uwezekano kwamba simu yako ilikuwa imewaka
wakati inadondoka kwenye maji, kama maji yakiingia ndani mfumo wa umeme
unaweza kuharibika kwa kupiga shoti. Sasa fuata hatua hizi
Zima simu yako
Ukishazima hatua muhimu inayofuata ni kutoa vitu
vyote kwenye simu kama betri, kasha, kadi na vitu vingine ambavyo
vinatumika kwenye matumizi ya simu yako.
Itingishe
Tingisha simu yako juu na chini hasa sehemu za
kuingiza umeme au kuchomeka kifaa cha kutoa picha au video au kifaa cha
kuchomeka visikilizio na sehemu za kubonyeza.
Baada ya kutingisha tumia kitambaa laini , pamba au sponji kukausha maji yaliyopo kwenye simu yako kama yaliingia.
Iweke ndani ya mchele
Kama una mchele kwenye mfuko au chombo maalumu,
iweke simu yako halafu funika kisha weka kwenye sehemu iliyokauka hii
itasaidia kunyonya maji maji na mengine kwenye kifaa chako .
Acha simu yako ndani ya mchele kwa saa 24 mpaka 48, usijaribu
kuiwasha au kuishika muda wote huo kuona kama imeanza kufanya kazi au
la. Kama haikuwa na maji mengi ndani ya muda huo, itaanza kufanya kazi.
Weka akilini kwamba si lazima simu yako iwake
baada ya kufanya yote hayo, kuna uwezekano wa asilimia 50 tu wa simu
yako kuwaka na kufanya kazi tena.
Peleka kwa mtaalamu
Kama imeshindikana kuwaka baada ya jitihada zote
hizo ni vizuri upeleke kwa wakala aliyeidhinishwa kuuza au kutengeneza
simu husika kama umenunua kwake
Pamoja na maelezo yote hapo tu, unatakiwa ujiandae na ujue njia za kuikinga simu yako dhidi ya maji siku nyingine .
Kama unatembea sehemu za mvua au maji maji kama
baharini, mto au bwawani unaweza kununua mfuniko usioingia maji kwa
ajili ya kukinga simu yako
Mifuniko hii ina sehemu unayoweza kuangalia kama kuna simu imeingia, ujumbe au kitu kingine.
Suala la simu yako kuingiliwa na maji au kupata
tatizo la umeme, mara nyingi halipo kwenye ‘warranty’ ili kuweza kupata
faida ni bora kuwa na bima ya simu na vifaa vingine vya elekroniki ili
inapopata shida iwe rahisi kupata nyingine kuliko kutumia gharama kubwa
kununua kifaa kingine.
Muhimu ni kujua na kuzingatia suluhisho hili.
Lakini njia nzuri zaidi ni kupeleka simu yako kwa fundi au mtaalamu wa
simu ili aweze kuingalia na kufanya marekebisho kama kuna uwezekano huo.
Kuendelea kutumia simu mbovu au zenye shida fulani
zinaweza kukuletea madhara ya kiafya, kwa sababu kuna vifaa ndani ya
simu vinaweza kufanya kazi ndivyo sivyo. Vifaa hivi ni kama kioo, mfumo
wa sauti na mfumo wa umeme. Natoa tahadhari kwa watumiaji wa simu wenye
mazoea ya kuchokonoa vifaa hivyo pasina ujuzi wowote. Hiyo ni kazi ya
fundi.