Header ads

Header ads
» » UDOM kinatarajiwa kufanya hafla ya kumuenzi Rais Jakaya Kikwete

 
CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM) kinatarajiwa kufanya hafla ya aina yake ya kumuenzi Rais Jakaya Kikwete.
Kitamuenzi kama sehemu ya kutambua mchango wake wa hali na mali, uliofanikisha kuanzishwa kwa chuo kikuu hicho cha aina yake Tanzania na nje ya Tanzania.
Taarifa ya kusudio la chuo hicho kumuenzi Rais Kikwete, limetolewa mwishoni mwa wiki na Makamu Mkuu wa UDOM, Prof. Idris Kikula wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mabalozi na Maofisa wa Uwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
Profesa Kikula na ujumbe wake yuko katika ziara ya kikazi nchini Marekani. Ziara hiyo ilimfikisha jijini New York, ambapo ujumbe ulipata fursa ya kukagua vifaa tiba na vitabu vya kiada na ziada, ambavyo vimetolewa na wadau mbalimbali wenye mapenzi mema na Tanzania.
Baada ya kukagua vifaa na vitabu hivyo na kujiridhisha, Makamu Mkuu wa UDOM ameushukuru Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwa kuwapatia fursa hiyo ya kujionea wenyewe aina ya vifaatiba na vitabu, ambayo amesema vitakuwa msaada mkubwa kwa Kitivo cha Sayansi ya Afya cha Chuo hicho.
“Waheshimiwa Mabalozi, mimi na ujumbe wangu napenda kwa moyo wa dhati kabisa kutoa shukrani zetu kwa kutuonesha vifaa na vitabu ambavyo kupitia kwenu wafadhili wamevitoa kuwasaidia watanzania nanyi mkaona bora kutushirikisha na kuona namna gani chuo chetu kinaweza kunufaika na misaada ya aina hii,” alisema Profesa Kikula.
Aliongeza kuwa Kitivo cha Sayansi ya Afya na ambacho pia kina zahanati, kinahitaji sana misaada ya kila aina ili kiweze kutimiza lengo lake kuu la kuwaandaa madaktari na wataalamu mbalimbali, lakini pia kutoa huduma uchunguzi na matibabu siyo tu kwa wanafunzi na wafanyakazi wa UDOM bali pia kwa Watanzania wote.
“Uongozi wangu unapenda kutambua juhudi zenu hizi za kushirikiana na wadau mbalimbali kusaidia siyo tu vyuo vikuu vyetu, lakini na watanzania. Mmedhihirisha kwa vitendo na si maneno na hii imetupa faraja sana na kudhihirisha namna gani tunaweza kushirikiana kwa karibu zaidi."
Alisema kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dodoma ni ndoto na hatimaye mbegu iliyopandwa na Rais Kikwete, ndoto uliyoanzia kwenye kampeni yake ya urais mwaka 2005.
“Ilianza kama ahadi ya kampeni, ahadi ambayo haikuishia katika maneno matupu ya ahadi bali aliitekeleza ahadi ile na leo hii tunaiona mbegu aliyoipanda ikichanua na mavuno yanaonekana,” alisema Prof. Kikula kwa msisitizo wa aina yake.
Anasema haikuwa rahisi kuifanikisha ndoto ya Rais kutokana na pingamizi mbalimbali kutoka nje na ndani ya serikali.
“Niseme kwamba haikuwa kazi rahisi, tulipata wakati mgumu na pingamizi hata kutoka ndani ya serikali. Wapo baadhi ya viongozi ambao hawakutaka Chuo Kikuu hiki kijengwe Dodoma. Mimi binafsi nilimuuliza Rais kwa nini alikuwa anataka Chuo Kijengwe Dodoma? akanijibu; “Ninataka kijengwe Dodoma na si kwingine, kwa sababu kwanza, ya umaskini wa Mkoa wa Dodoma na pili Dodoma ni Makao Makuu ya Nchi”.
Balozi Tuvako Manongi, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, ameushukuru uongozi wa UDOM kwa kuitikia mwito wa Uwakilishi wa kutumia ziara yao ya kikazi, kujionea kukagua vifaa na vitabu ambavyo vimepatikana kwa ushirikiano wa uwakilishi na wadau mbalimbali.

Imehaririwa na;- poatel Africa

Habari yako! Endelea kutembelea Tovuti ya TeknoTaarifa kwa Taarifa murwa za Teknolojia kutoka ndani na nje ya Tanzania, Tupo kwa ajili ya wapenzi wa Teknolojia.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post