Rufiji/Dar. Jeshi la Polisi Tanzania, limekumbwa na janga la tatu katika kipindi kisichozidi miezi saba baada ya watu wanaosadikiwa kuwa majambazi kuvamia na kuua askari wake wawili katika Kituo cha Ikwiriri wilayani Rufiji juzi na kisha kupora bunduki saba na risasi 60.
Tukio hilo limefanya jumla ya askari waliouawa
kufikia watano huku bunduki 22 na risasi zaidi ya 120 zikiwa zimeporwa
baada ya kuvamiwa kwa vituo vitatu vya polisi tangu Juni 11 mwaka jana.
Mbali na Ikwiriri, vituo vingine vilivyovamiwa ni Mkamba Kimanzichana, Mkoa wa Pwani na Bukombe mkoani Geita.
Matukio hayo yametokea ikiwa ni mwaka mmoja na
wiki tatu tangu Ernest Mangu alipoanza kazi ya Inspekta Jenerali wa
Polisi (IGP) akimrithi mtangulizi wake, Said Mwema.
Tukio la juzi
Watu 15 wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wakiwa na
silaha za kivita na mabomu ya kurusha kwa mkono walivamia Kituo cha
Ikwiriri ambacho ni kikubwa kuliko vyote wilayani Rufiji ambacho pia ni
makao makuu ya polisi ya wilaya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei
alisema tukio hilo ambalo ni la pili kutokea katika kipindi cha miezi
saba mkoani humo, Koplo Edgar Milinga wa Kikosi cha Usalama Barabarani
aliuawa kwa kukatwakatwa mapanga na mwenzake, Judith Timoth alipigwa
risasi na kufariki dunia.
Kamanda Matei alizitaja silaha zilizoporwa kuwa ni
SMG mbili, Shortgun moja, SR mbili na bunduki za kurushia mabomu ya
machozi mbili. Kamanda Matei aliapa kuwasaka majambazi hao.
Ilivyokuwa
Habari zilizopatikana kutoka eneo la tukio
zimesema kuwa majambazi hao walivamia kituo hicho saa nane usiku na
kuwakuta askari hao wawili na kuwapiga risasi.