Katibu mtendaji wa Baraza la Mitihani la taifa,Dk Charles Msonde
Dar es Salaam. Juhudi za Serikali kuinua ufaulu wa masomo ya sayansi katika elimu ya sekondari sasa zitakuwa zimepata picha halisi ya hali ilivyo baada ya matokeo ya mtihani wa kidato cha pili kuonyesha ufaulu mdogo katika masomo hayo na mwanafunzi mmoja tu akipata alama zote katika somo la bailojia.
Dar es Salaam. Juhudi za Serikali kuinua ufaulu wa masomo ya sayansi katika elimu ya sekondari sasa zitakuwa zimepata picha halisi ya hali ilivyo baada ya matokeo ya mtihani wa kidato cha pili kuonyesha ufaulu mdogo katika masomo hayo na mwanafunzi mmoja tu akipata alama zote katika somo la bailojia.
Hata hivyo, matokeo ya kidato cha pili
yaliyotangazwa jana na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), yanaonyesha
ufaulu mkubwa kwa matokeo ya masomo yote kwa jumla.
Kati ya watahiniwa 453,191 waliosajiliwa kufanya
mtihani huo Novemba 24 hadi Desemba 5 mwaka jana, ni watahiniwa 405,204
sawa na asilimia 89.0 waliofanya mtihani na watahiniwa 47,987 sawa na
asilimia 10.60 hawakufanya.
Kati ya watahiniwa hao, wasichana walikuwa 233,834 sawa na asilimia 51.60 na wavulana 219,357 sawa na asilimia 48.40.
Akitangaza matokeo hayo jana jijini hapa, Katibu
Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema: “Somo ambalo limefanya
vibaya zaidi ni hisabati... Walifanya wanafunzi 381,973 na waliofaulu ni
69,332 sawa na asilimia 18.15, sayansi ya kilimo waliofanya walikuwa
18,946 na waliofaulu ni 6,526 sawa na asilimia 34.45.”
Alifafanua kuwa jumla ya watahiniwa 375,434, sawa
na asilimia 92.66 ya waliofanya mtihani mwaka jana, wamepata alama
zinazowawezesha kuendelea na masomo ya sekondari ya kidato cha tatu.
“Kati yao wasichana ni 195,328 sawa na asilimia
92.63 na wavulana ni 180,106, sawa na asilimia 92.69. Watahiniwa 29,770
sawa na asilimia 7.34 wamepata alama ambazo baraza limeona ni bora
wakarudia darasa,” alisema Dk Msonde.
Alisema: “Mwaka 2013 watahiniwa waliopata alama za
kuendelea na kidato cha tatu walikuwa 422,446 sawa na asilimia 89.34 ya
watahiniwa 472,833 ya waliofanya mtihani huo.”
Pia, alieleza kuwa katika mtihani wa kemia,
waliofanya mtihani walikuwa 399,725 na waliofaulu ni 153,613, sawa na
asilimia 38.43. Waliofanya somo la fizikia walikuwa 398,502 na
waliofaulu ni 154,318 sawa na asilimia 38.72 wakati somo la biashara
walikuwa 78,331, waliofaulu ni 33,411 sawa na asilimia 42.65.
Alimtaja Sophia Boneka kutoka Sekondari ya
Heritage Dar es Salaam kuwa ndiye aliyepata alama 100 katika somo la
biolojia kati ya watahiniwa 400,105, huku akishika nafasi ya 10 kati ya
381,973 kwenye somo la hisabati.
Dk Msonde alisema somo la uraia aliyepata alama
100 ni mmoja kati ya watahiniwa 378,139 ambaye ni Martine Jackson kutoka
Shule ya Sekondari Moshi mkoani Kilimanjaro.
Alisema: “Tatizo la masomo haya kufanya vibaya
linaweza kuangaliwa kwa mapana zaidi, labda kuna matatizo kwa walimu
wanaowafundisha au wanafunzi wenyewe hivyo ni jukumu la wadau kulitazama
hili.”