Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ardhi Dar es Salaam (ARU) Juvenal Shirima amepandishwa kizimbani akikabiliwa na kosa la kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa WhatsApp.
Mshtakiwa huyo alisomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Godfrey Mwambapa na wakili wa Serikali, Adolf Mkini ambapo Mkini alidai kuwa mshtakiwa January 13 2017 kupitiaWhatsApp Group la ‘Lowassa Foundation and Bunge Live‘ alichapisha taarifa za uongo.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo alikana kuhusika na kosa hilo ambapo Wakili Mkini alisema upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na hana pingamizi na dhamana.
Hakimu Mwambapa alimpa masharti ya dhamana mshtakiwa huyo ya kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya milioni mbili kwa kila mmoja pamoja na barua ambapo hata hivyo mshtakiwa huyo alitimiza masharti hayo ya dhamana na kesi imeahirishwa hadi February 9 2017