Uchumi usio wa pesa taslimu wa Rwanda umepigwa jeki ,huku Benki ya KCB Rwanda ikijiandaa kuanzisha mfumo mpya wa malipo ambao unatarajiwa kupanua huduma za kidijitali na huduma za utumaji pesa kwa njia ya simu nchini humo.
Mfumo huo mpya uitwao mVisa utaharakisha ufanisi na ubora wa mifumo ya ulipaji nchini Rwanda,na pia kupunguza gharama za uendeshaji nchini humo.
Mkurugenzi Mkuu wa benki ya KCB Rwanda Maurice Toroitich amesema jukwaa hilo litaharakisha juhudi za kuibadilisha Rwanda kuwa nchi isiyotumia pesa taslimu.
Alisema uwekezaji katika dijitali na utumaji pesa kwa njia ya simu pia utapunguza gharama za kufanya biashara nchini Rwanda na katika kanda .
Mpango huu wa kuanzisha huduma za mVisa ni sehemu ya suluhisho la uvumbuzi wa malipo kwa njia ya simu ambao utapiga jeki ufanisi na kuhakikisha kuwa wateja wanafurahia mbali na kupunguza gharama za malipo.