Kitendo cha Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwenda katika Kituo cha Mabasi cha Ubungo (UBT) kuwashawishi madereva kusitisha mgomo kimepokewa kwa hisia tofauti na wananchi.
Wakizungumza jana, baadhi ya wananchi walisifu kitendo hicho huku wengine wakisema alikuwa akitafuta umaarufu wa kisiasa.
Hata hivyo, Mbowe aliwaambia waandishi wa habari
kwenye makao makuu ya Chadema kuwa aliamua kwenda kuzungumza na madereva
hao kwa nia ya kuwaeleza kuwa mgomo wao unazidi kuwatesa wananchi na
kwa kuwa ujumbe wao ulishafika.
Alisema Serikali imeshindwa kutatua matatizo ya
wananchi na hivyo migomo inahitajika ili kuisukuma Serikali kutatua
matatizo ya wananchi.
“Mgomo huo ni matokeo ya Serikali kupuuza madai
yao kwa muda mrefu na kauli aliyoitoa (mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,
Paul) Makonda inaonyesha ni aina gani ya viongozi tuliona nao hapa
nchini. Wamekosa majibu ya kumaliza tatizo hilo,” alisema.
Mbowe alisema hata kitendo cha Makonda kuahidi
kushughulikia matatizo ya madereva ifikapo leo na yasipotatuliwa
ataungana nao, ni hatari.
“Haya ni matokeo ya kuwa na viongozi wasio na sifa,” alisema Mbowe.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa
wamechukulia kitendo cha mwenyekiti huyo wa Chadema kuwa ni cha
kujitafutia umaarufu kirahisi.
Mhadhiri mwandamizi ambaye ni Mkuu wa Idara ya
Sayansi ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Emmanuel Mallya
alisema katika mazingira kama hayo siyo jambo la ajabu kuona mwanasiasa
akijitokeza.
“Mwanasiasa yeyote anapoona migogoro kama hiyo, ni
rahisi zaidi kuitumia nafasi hiyo ili kujijengea mazingira mazuri ya
kukubalika kisiasa, iwe kwa nia nzuri au vinginevyo kutokana na udhaifu
uliojitokeza,” alisema Mallya.
Mallya alisema mgomo huo haukutakiwa kuchanganywa na itikadi za kisiasa kutokana na unyeti wake.
“Siyo jambo la kupendekeza kwa chama chochote cha
kisiasa kutaka kugeuza mgomo huo kuwa ajenda ili kujinufaisha kisiasa,”
alisema.