Header ads

Header ads
» » Simba yapewa siku nane za kufuta aibu Ligi Kuu Bara



SIMBA ina siku nane kuanzia leo Ijumaa mpaka Aprili 3 kujiandaa na kujiweka sawa kabla ya Ligi kuendelea.

Kocha Goran Kopunovic amesisitiza kwamba muda huo unamtosha kuiweka Simba sawa tayari kurudi kwenye fomu kupambana kusaka nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa ligi.

Simba itacheza na Kagera Sugar ugenini, Aprili 4 siku ambayo Yanga itakuwa Zimbabwe kurudiana na Platinum kwenye Kombe la Shirikisho.




Simba ilitarajiwa kujificha katika Hoteli ya Upland iliyopo Changanyikeni jijini Dar es Salaam ambapo itakuwa ikijiandaa na mechi hiyo ngumu kwao kutokana na historia wanapokwenda kucheza na Kagera ambapo mara nyingi hupoteza ama kutoka sare.

Hii itakuwa ni mara ya pili msimu huu Simba kwenda kucheza kwenye uwanja huo baada ya mechi yao ya awali ilipocheza na Stand United na kufungwa bao 1-0 jambo ambalo limewafanya viongozi wa Simba kuwa na tahadhari kubwa hususan katika mechi za Kanda ya Ziwa.

Hata hivyo, Simba itakuwa na kazi kubwa kuhakikisha inashinda mechi tatu mfululizo kama ilivyopanga ambapo baada ya Kagera itarudi jijini Dar es Salaam kucheza na Ruvu Shooting huku ikibakiwa na mtihani mkubwa wa ugenini dhidi ya Mbeya City, mechi itakayochezwa Aprili 18 Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Mechi yao na Mbeya City itakuwa ngumu kwani ni timu inayotaka kujinasua kushuka daraja baada ya kupata matokeo mabaya kwenye mechi zilizopita. Mbeya City inashika nafasi ya tisa ikiwa na pointi 23.

Tangu Wekundu hao wa Msimbazi wafungwe na Mgambo mabao 2-0, viongozi wamekuwa na vikao vya mara kwa mara vya kuhakikisha wanafanya vizuri mechi zijazo japo waweze kushika nafasi ya pili kwenye ligi ili kushiriki michuano ya kimataifa.

Mazoezi ya timu hiyo yanafanyika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam huku Kocha wa Simba, Goran Kopunovic akiwa na imani kubwa na kikosi chake kupata ushindi katika mechi zijazo. Endapo itashinda mechi hiyo itafikisha pointi 35 lakini bado itakuwa nyuma ya Azam.

Awali Simba ilikuwa inapigania kutwaa ubingwa lakini imeonekana ni mgumu kwao kwani tayari Yanga imewaacha kwa pointi nyingi ambapo imefikisha pointi 40 na ina mechi moja mkononi wakati Simba ina pointi 32 ikiwa imecheza mechi 20 huku Kagera inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 24.

Hata hivyo, Simba ina nafasi ya kushika nafasi ya pili endapo Azam ambayo inashika nafasi hiyo kwenye msimamo ikiwa na pointi 37 itakubali kupoteza mechi nne kati ya nane zilizobaki.

Simba imebakiza mechi sita na ili ipate nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa basi inatakiwa ifikishe pointi 50 kwa kufanya kazi ngumu ya kushinda michezo yake yote iliyobaki katika ligi hiyo inayoelekea ukingoni.

Imehaririwa na;- Unknown

Habari yako! Endelea kutembelea Tovuti ya TeknoTaarifa kwa Taarifa murwa za Teknolojia kutoka ndani na nje ya Tanzania, Tupo kwa ajili ya wapenzi wa Teknolojia.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post