Header ads

Header ads
» » Ngassa: Nimepata timu Qatar



BAADA ya kutoa kauli kuwa anaondoka Yanga, hatimaye kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Mrisho Ngassa, amefunguka juu ya kule anapoelekea baada ya kuondoka klabuni hapo.

Ngassa ameliambia gazeti hili katika mahojiano maalum kuwa, kuna timu tatu za nchi tatu tofauti ambazo anafanya nazo mazungumzo na muda wowote anaweza kumalizana na mojawapo, kisha atataja rasmi anaenda klabu ipi kwa kuwa mkataba wake na Yanga umebakiza muda mfupi.

Ngassa amefikia uamuzi huo baada ya kudai kuwa uongozi wa klabu umegoma kulipa deni la shilingi milioni 45 alilokopa benki wakati akitua klabuni hapo akitokea Simba baada ya kukiuka kanuni za uhamisho.
Ngassa amesema kuwa nchi ambazo kuna timu anamalizana nazo ni Qatar, Afrika Kusini na DR Congo.

“Nina asilimia tatu za kubaki Yanga, lakini asilimia zilizobaki zote ni kuwa sitaongeza mkataba wa kuichezea klabu hiyo, namalizia muda uliobaki kiungwana kisha akili yangu nitaielekeza kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi,” alisema Ngassa.




“Naipenda Yanga na nitaitumikia kwa moyo mmoja katika muda huu uliosalia wa mkataba wangu, ndiyo maana umeona hata mechi ya jana (juzi) nilicheza vizuri na kusaidia ushindi tulioupata (dhidi ya JKT Ruvu).
“Siwezi kutaja majina ya klabu hizo kwa sasa ambazo nafanya nazo mazungumzo lakini zinatoka DR Congo, Qatar na Sauz.

“Mazungumzo yanaendelea vizuri na kwa moyo mmoja nimeamua kwenda nje ndugu yangu, nahisi akili yangu imechoka kucheza hapa nchini kwa sababu nakutana na mambo na vitu vilevile tangu nilipotoka Azam FC, Simba na hapa Yanga,” alisema Ngassa.

Alipoulizwa juu ya hatima ya Ngassa kuondoka klabuni hapo, Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha alifafanua kuwa hawamzuii yeye wala mchezaji mwingine yeyote ambaye anataka kuondoka ilimradi afuate taratibu za klabu, kauli ambayo inamaanisha kuwa hawana kipingamizi tena cha mchezaji huyo kuondoka.

Wachezaji wa Yanga ambao wapo kwenye miezi ya mwisho kumaliza mikataba yao klabuni hapo na hakuna tamko lolote kutoka kwa uongozi wa klabu, juu ya kuwaongezea mikataba ni Deogratius Munishi ‘Dida’, Hassan Dilunga, Hussein Javu, Said Bahanuzi, Rajabu Zahir, Nizar Khalfan, Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite.

Imehaririwa na;- Unknown

Habari yako! Endelea kutembelea Tovuti ya TeknoTaarifa kwa Taarifa murwa za Teknolojia kutoka ndani na nje ya Tanzania, Tupo kwa ajili ya wapenzi wa Teknolojia.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post