Simba imejipigia Ruvu Shooting mabao 3-0, jijini Dar es Salaam huku mabingwa watetezi Azam wakifuata nyayo za Yanga kupata ushindi uwanjani Mkwakwani, Tanga.
Simba ilifunga kupitia kwa Ibrahim Ajibu aliyefunga mkwaju wa penalti dakika ya 60 baada ya mtokea benchi Awadh Juma ‘Maniche’ kuangushwa na mabeki wa Ruvu wakati akielekea kufunga. Bao la pili la Simba ndilo lililokuwa tamu baada ya Awadh kuwafunga tela mabeki wa Ruvu na kufumua shuti kali ambalo lilimbabatiza mmoja wa mabeki wa maafande hao na kutinga wavuni. Elias Maguli aliyeingia uwanjani kipindi cha pili kumpokea Emmanuel Okwi aliiandikia Simba bao la tatu katika dakika ya 75 baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Abdallah Abdallah aliyekuwa ameokoa shuti kali na Said Ndemla.
Kwa ujumla pambano la jana ambalo awali mashabiki walijua litaahirishwa kutokana na mvua kubwa zinazoendelea Dar es Salaam, lilichezwa kama kawaida baada ya mvua kukata saa nzima kabla ya mchezo kuanza. Timu zote zilipoteza nafasi nyingi za wazi Simba wakiongoza kwa kupoteza kupitia kwa Emmanuel Okwi ambaye jana hakuwa na bahati katika mchezo huo pamoja na Ramadhani Singano ‘Messi’, na Ajibu.
Ruvu ambayo walionyesha uhai kwa kiasi walilitia kashkash lango la Simba, lakini uimara na umakini wa kipa Manyika Peter uliifanya timu hiyo kuambulia patupu. Kipindi cha pili hasa baada ya Simba kupata penalti hiyo iliyoonekana imejaa utata, wachezaji wa Ruvu walipoteza umakini wao na kuwapa nafasi wapinzani wao kuwakimbiza na kupata ushindi huo ambao umewafanya Simba kujikita kwenye nafasi ya tatu kwa kufikisha pointi 32 huku Azam ikifikisha pointi 33 baada ya kuichapa Coastal Union bao 1-0, huku waamuzi wakitolewa uwanjani chini ya ulinzi wa Polisi baada ya mashabiki wa Coastal kutaka kuwapiga kwa madai waliionea timu yao.
Bao pekee katika pambano hilo la Tanga lililokuwa kali liliwekwa kimiani na John Bocco ‘Adebayor’ katika dakika ya 32 baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Coastal na mpira kumkuta Shomari Kapombe aliyepiga shuti lililowababatiza mabeki wa Wagosi na mpira kumkuta Bocco aliyefumua shuti kali lililotinga wavuni. Katika mchezo mwingine Prisons ilitoka suluhu na Polisi Morogoro mjini Mbeya.