Kampuni ya Conceptos Plasticos ya Colombia imevumbua njia nzuri ya kujenga nyumba kwa takataka za plastiki. Si kama tu inaweza kutatua tatizo la uchafuzi wa takataka za plastiki, bali pia inaweza kuwasaidia watu maskini wapate nyumba zao.
Kampuni hiyo inatengeneza matofali mepesi yasiyoweza kushika moto kwa kuyeyusha takataka za plastiki na mpira, kuongeza kemikali fulani na kuziweka kwenye kalibu. Tofauti na matofali ya kawaida, matofali hayo yanafanana na yale ya LEGO ambayo yana ulimi na tundu unganishi, hivyo watu wanapojenga kwa matofali hayo hawana haja ya kutia gundi au saruji, hata watu wasio na uzoefu wa kujenga wakipata mafunzo kidogo wataweza kujenga nyumba zao wao wenyewe. Kwa mfano, kujenga nyumba ya mita 40 za mraba yenye vyumba viwili vya kulala, choo, sebule, jiko na ukumbi wa kulia kunahitaji watu wanne wasio na uzoefu kujenga kwa siku tano. Aidha, nyumba zinazojengwa kwa matofali hayo zinaweza kupasuliwa, kuhamishwa na kujengwa upya wakati wowote.
Mwanzilishi wa kampuni hiyo Bw. Oscar Mendez alisema uvumbuzi huo ni muhimu kwa jamii, kwani asilimia 40 ya watu katika nchi za Afrika, Latin Amerika na Asia hawana nyumba, anatarajia kampuni yake itawasaidia watu hao wapate nyumba za bei rahisi.
Uvumbuzi huo pia utaleta faida ya kiuchumi na manufaa kwa mazingira. Bw. Mendez alisema katika mji wa Pogota, asilimia 12 ya takataka ni plastiki, lakini ni asilimia 13 tu ya takataka za plastiki zimetumiwa tena, kampuni yake imezifanya takataka hizi ziwe na thamani tena.
Chanzo: wonderfulengineering.com