Timu ya kampeni ya Chama cha Democratic nchini Marekani imesema kompyuta inayotumiwa kuratibu kampeni za mgombea wao, Hillary Clinton imedukuliwa. Tukio hilo limekuja siku chache baada ya chama hicho kumaliza mkutano wake mkuu uliofanyika Philadelphia kwa Clinton kuidhinishwa rasmi kuwa mgombea urais wa Marekani katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Novemba mwaka huu.
Mkutano huo ulifanyika wiki moja baada ya kumalizika kwa mkutano wa Republican ambao uliibua mjadala mkubwa baada ya mke wa Donald Trump, Melania kudaiwa kuiba hotuba iliyotolewa miaka minane iliyopita na Michelle Obama. Jana, timu hiyo ya Clinton ilieleza kuwa kitendo hicho kimefanywa kwa lengo la kuvuruga mwenendo wa kampeni za mgombea wao anazoendelea kufanya Pennsylvania. Katika kampeni zake,
Clinton amekuwa akiambatana na mumewe, Bill na mgombea mwenza, Tim Kaine.
Maofisa wa Clinton waliishutumu kambi ya kampeni ya mgombea urais wa Republican Trump kwa udukuzi huo. Chama hicho kimethibitisha uhalifu huo na kusema wadukuzi waliingia katika mfumo unaofanya tathmini ya wapigakura kwa kipindi cha siku tano
Chanzo: abc7news.com