Mageuzi na uvumbuzi wa teknolojia ni muhimu katika sekta ya nishati
Mkutano wa mwaka wa kimataifa kuhusu nishati CERAWeek ulifanyika wiki iliyopita huko Houston, nchini Marekani, ambapo wadau wa nishati duniani walijadili mikakati baada ya kufikiwa kwa makubaliano ya Paris kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa. Wadau hao wamesema mageuzi na uvumbuzi wa teknolojia ni muhimu kwa sekta za nishati za jadi katika kukabiliana na bei ndogo ya mafuta na changamoto zinazotokana na nishati safi, pia ni sehemu muhimu katika juhudi za kimataifa za kubana matumizi ya nishati na kupunguza utoaji wa hewa zinazosababisha ongezeko la joto duniani.
Kama kampuni nyingine za nishati, kampuni ya Chevron yenye makao yake makuu huko California, Marekani, inashuhudia kipindi kigumu. Ikikabiliwa na bei ndogo ya mafuta na wito wa kupunguza matumizi ya nishati na utoaji wa hewa chafu, kampuni hiyo inatafuta fursa za kufanya ushirikiano na kampuni ndogo na zenye ukubwa wa kati zinazozingatia uvumbuzi, hatua ambazo zinaweza kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza ufanisi wa matumizi ya rasilimali.
Mwezi uliopita, kampuni ya Chevron na kampuni ya mafuta na gesi ya Airborne zilisaini makubaliano ya kufanya ushirikiano wa kusanifu na kutengeneza bomba la kusafirishia mafuta kwenye bahari ya mbali ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza usalama.
Mtendaji mkuu wa kampuni ya mafuta na gesi ya Airborne Eric van der Meer amesema kampuni kubwa za nishati na kampuni za uvumbuzi zinaweza kusaidiana katika utafiti na usanifu na kupata mafanikio ya pamoja kupitia ushirikiano.
"Ni vigumu kwa kampuni zenye nguvu katika sekta fulani kufanya uvumbuzi, kwa kuwa wana mambo mengi ya kufuatilia. Uvumbuzi unahitaji juhudi zisizokoma na makosa, lakini cha muhimu ni kuwa na moyo wa uvumbuzi. Hiyo ndiyo nafasi inayochukuliwa na kampuni za uvumbuzi. Wakati huohuo kama kampuni zile kubwa zisipofanya uwekezaji, hatuwezi kufanya chochote."