Mnikulu Shaban Gurumo amekiri mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, kwamba alipokea Sh milioni 80.8 kutoka kwa James Rugemalira na kuzitumia kwa matumizi yake binafsi, ingawa amekanusha kuomba fedha hizo.
Gurumo
alitoa utetezi huo Dar es Salaam jana mbele ya baraza baada ya kusomewa
mashitaka ya kutumia cheo chake cha uongozi wa umma vibaya na kujipatia
fedha hizo, jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa
Umma.
Alikiri
kumfahamu Rugemalira, akisema ni rafiki yake kwa zaidi ya miaka 10.
Alisema daktari wake, Fred Limbanga ndiye aliyemtambulisha kwa
Rugemalira.
“Kama
Mnikulu sijawahi kupokea fedha za kiuchumi kwa Rugemalira wala kuwa na
mahusiano naye ya kiuchumi, naitambua akaunti ya Mkombozi kuwa ni ya
kwangu na niliifungua baada ya James kunishauri,” alisema Gurumo.
Alisema
awali hakufahamu nani aliyemwekea kiasi hicho cha fedha kwenye akaunti
hadi hapo baadaye alipotambua kuwa ni Rugemalira. Alidai hadi sasa
hajafahamu sababu za kupewa kiasi hicho cha fedha na wala hakuhangaika
kumuuliza Rugemalira.
Pia, alisisitiza kuwa pamoja na kutofahamu fedha hizo alipewa za matumizi gani, ana uhakika si zawadi kama inavyodaiwa.
“Ila
nahisi baada ya kuitwa na Kamati ya Uchunguzi ya Sekretarieti ya
Maadili ya Viongozi wa Umma kujibu tuhuma zinazonikabili, huenda
Rugemalira alinitumia fedha hizo baada ya kusikia kuwa nina mgonjwa
anayeumwa saratani ya mfuko wa uzazi,” alisema.
Alisisitiza
kuwa hajawahi kuzungumza wala kuomba fedha si kwa barua, simu wala kwa
mazungumzo ya ana kwa ana na Rugemalira, ila amekuwa akizitumia kwa
shughuli zake binafsi kwa kuwa alizikuta kwenye akaunti yake. “Sijawahi kuomba fedha yoyote kwa Rugemalira wala VIP,” alisema.
Alisema
pia hata katika tamko la mali na madeni, aliloliwasilisha Desemba 29,
mwaka jana kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, akiwa kama
kiongozi wa umma, aliziorodhesha fedha hizo kuwa ni mali yake iliyopo
katika akaunti yake ya Benki ya Mkombozi alizopewa na Rugemalira.
Alikiri
kuwa alikuwa na matatizo ya kuwa na mgonjwa huyo, aliyempeleka India
kwa matibabu na hadi sasa ameshatumia dola za Marekani 40,000 ambayo ni
sawa na Sh milioni 73.2, hivyo hakuwa na shida yoyote ya fedha. “Mimi
nina fedha zaidi ya hizo za Rugemalira ndio maana sikuomba.”
“Nakiri
kupokea fedha hizo Sh milioni 80.8, lakini nilishangaa kwa mara ya
kwanza niliposikia kwenye redio iliyokuwa ikirusha hewani kipindi cha
Bunge, mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alikuwa akisisitiza
nilipewa Sh milioni 800 na kampuni ya VIP Engineering and Marketing
Limited, jambo ambalo si la kweli,” alisema.
Aliomba
baraza hilo kuwachukulia hatua na kuwachunguza wale wote waliodanganya,
wakiwemo wabunge na vyombo vya habari pamoja na mitando ya kijamii,
kuhusu kiasi cha fedha alizopatiwa na Rugemalira ili ifahamike kama
wamefanya makusudi, wametumika au la.
Awali,
akimsomea mashitaka mbele ya baraza hilo, Mwanasheria wa Sekteratieti
ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Hassan Mayunga alidai mlalamikiwa akiwa
kiongozi wa umma, aliomba na kupokea Sh milioni 80.8 kutoka kwa kampuni
ya VIP kinyume cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Aidha
alidai mlalamikiwa huyo, alipokea kiasi hicho cha fedha kinyume cha
sheria hiyo, inayokataza kiongozi wa umma kuomba na kupokea fedha kwa
maslahi yake binafsi.
Alidai
Februari 5, mwaka jana alipokea Sh milioni 80.8 kutoka kwa VIP kupitia
akaunti yake namba 00110102645401 iliyopo katika Benki ya Mkombozi tawi
la St Joseph jijini Dar es Salaam.
Shahidi
upande wa Sekretarieti hiyo, ambaye ni Ofisa Uchunguzi, Bazilio
Mwanakatwe, alidai kupitia kamati ya uchunguzi iliyoundwa na
sekretarieti hiyo, walibaini Gurumo alikiuka maadili ya viongozi wa
umma, kutokana na kupokea kiasi hicho kikubwa cha fedha bila kukitamka
kwa viongozi wake ili kipangiwe matumizi.
“Sheria
inatamka wazi kuwa kiongozi wa umma haruhusiwi kuomba au kupokea zawadi
kubwa kwa maslahi yake isipokuwa zawadi ndogo isiyozidi Sh 50,000 na
endapo itazidi atatakiwa kutamka zawadi hiyo na kukabidhi kwa Ofisa
Masuhuli wake ili waweze kuipangia namna ya kuitumia zawadi hiyo,” alisema.
Alidai
kamati hiyo ilibaini pia uwepo wa mgongano wa malsahi ambapo Gurumo
ambaye ni Mnikulu wa Ofisi ya Rais, kwa nafasi aliyonayo anafahamu siri
nyingi na kupata fursa nyingi hivyo kitendo cha kupokea fedha kutoka kwa
mwekezaji mkubwa ni kujiingiza katika mgongano wa maslahi.
Kwa
upande wake, Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa
Umma, Getrude Cyriacus, alidai Gurumo, baada ya kuingiziwa fedha hizo,
hadi sasa ameshatoa na kutumia zaidi ya Sh milioni 77.
Hoja za kila upande kuhusu shauri hilo, zimepangwa kuwasilishwa tena mbele ya baraza hilo, Machi 13, mwaka huu.
Wakati
ofisa huyo wa Ikulu akiwa miongoni mwa viongozi wa umma watano
waliokwishafikishwa mbele ya baraza kwa madai ya kukiuka maadili, leo
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA),
Philip Saliboko, pia anapandishwa kizimbani kujibu mashitaka akidaiwa
kupatiwa Sh milioni 40.4 kutoka Kampuni ya VIP.
Wakati
huo huo, leo baraza hilo linatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu pingamizi
lililowasilishwa juzi na aliyekuwa Mkurugenzi wa Ushauri wa Kisheria wa
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma
aliyetaka shauri linalomkabili la kupokea Sh milioni 423, liahirishwe
kusikilizwa kutokana na kesi ya msingi iliyopo Mahakama Kuu.