Baraza la Mitihani
Tanzania (Necta) limesema usahihishaji wa mitihani ya kidato cha nne
uliofanyika Novemba mwaka jana, umekamilika.
Katibu mtendaji wa
Necta, Dk Charles Msonde alisema kuwa
“usahihishaji umekamilika na baraza lipo katika uchambuzi wa kuyapanga
na tutakapokamilisha tutayatangaza”.
Alipoulizwa ni lini hasa
matokeo hayo yatatangazwa, Dk Msonde alisema: “Tumemaliza kusahihisha
na mchakato wa kuyapanga ukikamilika tutawaeleza hivyo msiwe na shaka.”
Katika kipindi cha miaka
miwili mfululizo, mwaka 2012 na 2013, Necta ilitangaza matokeo ya
kidato cha nne mwishoni mwa Februari na mwanzoni mwa Machi.
Matokeo ya Mtihani wa
Kidato cha Nne uliofanyika mwaka 2013 yalitangazwa Februari 22, mwaka
jana na 2012 yalizua gumzo kutokana na asilimia 60 ya watahiniwa kufeli.
Kwa kawaida, muhula wa
masomo kwa kidato cha tano huanza Julai, huku Machi na Aprili mchakato
wa kuwapangia shule hufanyika wakati Mei na Juni hutumiwa kwa maandalizi
kwa wanafunzi hao.
Katika matokeo ya 2013
kama ilivyokuwa katika matokeo ya mwaka 2012, shule binafsi zilikuwa na
matokeo mazuri kulinganisha na za Serikali zilizokuwa zikitamba miaka ya
nyuma.
Kwa mujibu wa Necta,
matokeo ya mwaka 2013, shule kongwe za Serikali na zile za vipaji
maalumu, zilishindwa kuingia kwenye orodha ya shule 30 bora.
Shule kongwe kihistoria
zimekuwa zikitoka kapa katika matokeo ya Mtihani wa Taifa. Tofauti na
matarajio ya wengi, shule hizo nyingi hazikuwamo hata katika orodha ya
shule 100 bora.
Baadhi ya shule hizo ni
Fidel Castro ambayo ilishika nafasi ya 83, Malangali (172), Ifunda
Ufundi (205), Jangwani (226), Bwiru (242), Songea Wavulana (257), Pugu
(325) na Azania (333).
Ikiwa ni mwaka mmoja
umekamilika tangu Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ulipoanzishwa,
taasisi ya Hakielimu ilitoa matokeo ya utafiti wake yanayoonyesha hakuna
kilichofanyika.
Kaimu Mkurugenzi wa
HakiElimu, Godfrey Boniventura alisema Serikali isitumie kigezo cha
kuongezeka ufaulu kama ishara tosha ya kuimarika kwa elimu, kwani licha
ya ufaulu huu kuonyesha kupanda ghafla, kuna changamoto nyingi katika
sekta hiyo ambazo bado hazijatatuliwa na juhudi kubwa zinahitajika.
Via> Mwananchi