WATUMIAJI wa usafiri wa bajaji, bodaboda pamoja na teksi wametakiwa kutumia huduma mbadala na salama ya teknolojia rahisi ya usafiri ili kujiepusha na matendo ya wizi ambayo yanazidi kukithiri nchini.
Mwito huo umetolewa na Ofisa Mtendaji wa teknolojia inayomwezesha abiria kujipatia huduma za usafiri kirahisi kutokea mahala alipo ijulikanayo kama Twende App, Justin Kashaigili wakati akiizindua huduma hiyo jjini Dar es Salaam.
Kashaigili alisema abiria wengi wamekuwa wakipatwa na matatizo kadhaa wakiwa kwenye usafiri wa bodaboda, teksi na bajaji na kwa kutumia huduma ya Twende changamoto hizo zinatatuliwa.
Akielezea jinsi ya kujiunga na huduma hiyo, Kashaigili alisema, “abiria analotakiwa kufanya ni kupakua Twende App katika simu yake ambayo itamuunganisha na dereva moja kwa moja badala ya kuhangaika kwenda mwenyewe kufuata sehemu ilipo teksi.
Aliongeza, “huduma hii pia inatumia muda sahihi wa taarifa za dereva, mfumo hai wa satelaiti unaowezesha ramani ya kufahamu sehemu alipo abiria na kumuunganisha abiria mwenyewe na dereva aliyepo karibu na wakati huo huo kumwezesha dereva kutoa majibu.”
Akizungumzia huduma hiyo, Mkuu wa Zana za Kidijitali wa Tigo, Tawonga Mpore alisema, “Huduma hii ni kielelezo cha Tigo kujikita katika mageuzi ya mtindo wa maisha ya kidijitali kwa kutoa suluhisho kwa changamoto zinazowakabili wateja wake.