WATENDAJI wa Mahakama wametakiwa kuzingatia maadili ya kazi na kutumia teknolojia ya sasa kutoa haki kwa wananchi.
Aidha, Idara ya mahakama imesema inakusudia kuendelea kuboresha utunzaji kumbukumbu kwa njia ya kielektroniki ili kurahisisha huduma ya utoaji haki nchini.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA), Jaji Paul Kihwelo alipofungua mafunzo ya utunzaji wa kumbukumbu kwa njia za kisasa yanayoshirikisha makarani kutoka mahakama na maofisa wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(Tehama) wa Mahakama ya Tanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo, Mahakama ya Tanzania, Patricia Ngungulu alisema mafunzo haya ambayo yameshirikisha washiriki 51 yanalenga katika kuwajengea uwezo juu ya utunzaji wa kisasa wa kumbukumbu na kuongeza utendaji kazi wa haki kwa wananchi.
Mafunzo hayo yameshirikisha washiriki kutoka Dar es Salaam, Arusha, Manyara, Bukoba, Kibaha, Morogoro, Dodoma, Iringa, Njombe, Songwe, Sumbawanga, Shinyanga, Simiyu na Divisheni zote za Mahakama Kuu ambazo ni za Biashara, Kazi, Ardhi na Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.