Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi,
amesema serikali imeamua kufanya jitihada hizo baada ya kubaini
kutokuwapo kwa taasisi za kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini
kupata nyumba za gharama nafuu.
Alikuwa akizungumza katika warsha ya wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari.
Warsha hiyo iliandaliwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi chini ya mpango wake wa uwezeshaji wa umiliki ardhi.
Waziri Lukuvi alisema mpaka sasa bado haijapatikana taasisi iliyomudu
kujenga nyumba bora na za bei nafuu kwa wananchi wa kipato cha chini.
Alisema hata hizo zilizopo zinazotangaza kujenga nyumba za bei
rahisi, bado gharama zake ni kubwa na zimekuwa haziwaambii ukweli
wananchi kuhusiana na gharama za nyumba hizo.
“Tunafanya utafiti wa nyumba za gharama nafuu zaidi, tunatafuta
teknolojia ambayo itatusadia kuingia kwenye teknolojia ya kutusaidia
kufika huko.
Tumegundua kwamba hizi nyumba mpaka sasa katika nchi hii
hatujawezesha kuwa na nyumba za gharama nafuu na hata mimi sijaridhika
kwamba tumefikia kumudu kuwa na nyumba hizo,”
“Taasisi zinazojenga nyumba zimekuwa zikisema zinajenga nyumba za
gharama nafuu, lakini ukweli ni kwamba nyumba zinazojengwa si za gharama
nafuu, zinaitwa hivyo ni kwa majina tu, lakini ukweli ni kwamba
hatujamudu mahitaji ya kuwapatia wananchi nyumba za gharama nafuu, iwe
kwa ubora wake na thamani.
Tunataka mwaka huu tuingie kwenye teknolojia ambayo mtu ataona kweli
hii ni nyumba ya gharama nafuu, kwa ubora na thamani yake hasa kwa mtu
mwenye kipato cha chini.