UKUAJI wa masoko mtandao umebadilisha mazingira ya biashara ndogondogo nchini huku biashara ya magari imekuwa ikiongoza kunufaika na teknolojia hiyo, imebainishwa.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Stats. com, unaonesha kuwa biashara mtandaoni imekuwa kwa asilimia 40 ambao wataalamu wa uchumi wameshindwa kutabiri.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kupatana.com, Philip Ebbersten alisema jijini Dar es Salaam kuwa biashara ndogo na za kati zinachukua asilimia 70 ya biashara zote katika uchumi wa ndani, ambao unaonekana kuchagizwa na ukuaji wa teknolojia ya mtandao.
“Wakati viwanda vinaguswa na teknolojia ya mtandao, biashara ya magari ni miongoni mwa biashara iliyokuwa zaidi kutokana na teknolojia hii,” alisema.
Hapa nchini upatikanaji wa intaneti umekuwa ukiimarika kwa zaidi ya miaka 20 sasa, huku zaidi ya watanzania milioni tisa wanapata huduma hiyo, jambo linalochangia ukuaji wa biashara mtandao.
Ebbersten alisema ripoti ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania, inaonesha kuwa vyombo vya habari vya kidigitali, ikiwamo mitandao ya kijamii imechangia kuongeza ufanisi wa kuwafikishia bidhaa wateja wanaowataka.