Kwa kawaida wajasiriamali wengi hasa wadogo wadogo huzingatia mipango ya kukuza mitaji, kuimarisha uwezo wa wafanyakazi, kukuza faida, kuongeza wateja na matangazo. Lakini uwekezaji katika teknolojia inayoweza kuchagiza utekelezaji wa mipango na mikakati yao imekuwa siyo kipaumbele. Tofauti na mikakati mingine, teknolojia ni mtambuka katika biashara na haizuiliki ama kwa biashara ndogo au kubwa.
Teknolojia ni njia rahisi inayoweza kurahisisha ufanyaji kazi au utoaji wa huduma. Hivyo basi si vibaya kuwa na mikakati imara ya kuwekeza katika teknolojia. Chagua teknolojia inayokufaa. Uwekezaji katika teknolojia unategemea aina ya biashara na kiwango chake. Mfano; mfanyabiashara wa matunda anatakiwa kuzingatia teknolojia ya kuhifadhi matunda yasiharibike katika uchukuzi wake kutoka shambani na yakifika sokoni au dukani. Kwa mantiki hiyo, teknolojia nzuri ya uhifadhi iwe ya kienyeji au ya kisasa itasaidia malengo ya kukuza biashara. Hivyo, teknolojia ya majokofu ya kisasa yasiyo kula umeme mwingi au yanayotumia umeme wa jua itakuwa njia mwafaka.
Jambo la msingi ni kujenga utamaduni wa kufuatilia teknolojia inayokufaa kwa kuomba ushauri kwa wafanyabiashara walioendelea au kutafuta ushauri kwa wataalamu wa biashara kupata mawazo chanya. Pia, mtandao ni njia rahisi ya kujisomea kuongeza maarifa ya aina ya teknolojia unayoitaka. Baadhi ya teknolojia zinapatikana kwa bei ya juu na nyingine ni mchakato tu wa kwenda kujifunza kwa mfanyabiashara mwingine na kumlipa fedha kidogo.
Kwa sasa kuna vyuo vya ufundi stadi vinavyotoa kozi fupi za kuongeza ujuzi katika fani ya biashara. Kwa wafanyabiashara wadogo wanaweza kuanzisha vikundi na kuchangishana fedha za kumlipa mtaalamu awapatie teknolojia mpya inayoweza kukuza biashara zao na kuongeza vipato vyao. Tujaribu kuchukua mfano wa mafundi makenika. Hawa wanakumbana na teknolojia ya vyombo vya moto inayobadilika kila siku kutokana na mahitaji ya sasa ya kulinda mazingira, kupunguza matumizi ya mafuta, kuongeza starehe na mitindo.
Ili magari hayo yatengenezwe vizuri ni lazima fundi afahamu kidogo teknolojia iliyotumika kuyatengeneza. Lakini kama fundi alijifunzia kazi yake wakati magari ya Land Lover 109 yanabana mjini na hakujiendeleza ni lazima atashindwa kuhimili soko la ushindani wa sasa. Pia, vifaa vya utengenezaji na upimaji vinabadilika.
Badala ya kutumia jeki maarufu ya Tanganyika Jeki kunyanyua gari kwa sasa kuna teknolojia ya jeki rahisi zinazotumia nguvu ndogo. Hivyo, njia rahisi ya kwenda na soko ni kuwekeza katika ujuzi na vifaa.
>>Lengo langu ni kuakikisha upitwi na Habari za Teknolojia ungana Nami FACEBOOK , TWITTER na INSTGRAM