Kondoo huyo mwenye pamba za kilo 42.3 mwilini, anasemakana kupata matatizo ya kutembea kutokana na uzito wa pamba zake zilizochukua zaidi ya miaka ya mitano kuota.
Kondoo huyo alipatikana katika eneo la msitu uliokuwa karibu na mji wa Canberra nchini Australia.
Timu ya watu watano kutoka shirika la kulinda wanyama la RSPCA, walimgundua kondoo huyo msituni aliyekuwa amelemewa na pamba zake ndefu zenye upana wa sentimita 47.
Mkulima mmoja kwa jina la Ian Elkins alijitolea kunyoa pamba za kondoo huyo aliyebandikwa jina la Chris na mmoja wa wafanyakazi wa RSPCA.
Kwa kawaida wakulima huchukuwa muda wa dakika 3 pekee kunyoa pamba za kondoo zisizopita kilo 5 tofauti na za kondoo Chris zilizochukuwa muda wa dakika 45.
Kwa sasa kondoo Chris ndiye anayeshikilia rekodi mpya ya pamba nyingi duniani baada ya kuivunja rekodi ya kondoo Shrek wa New Zealand aliyekuwa na pamba za uzito wa kilo 27.