Header ads

Header ads
» » TUME ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imetangaza ratiba ya uchaguzi mkuu

 
TUME ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imetangaza ratiba ya kuanza kwa harakati za uchaguzi mkuu ambapo kuanzia wiki hii, fomu za kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar zitaanza kutolewa.
Hadi sasa ni vyama vitatu vya siasa vilivyotangaza kusimamisha wagombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar vikiwemo Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Wananchi (CUF) na ADC.
Kwa mujibu wa taarifa ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwenda kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Mwenyekiti wa Tume, Jecha Salim Jecha inaonesha kwamba utoaji wa fomu za urais utaanza Jumatatu hadi Septemba 6 hapo katika ukumbi wa Salama Inn uliopo hoteli ya Bwawani.
Aidha ratiba hiyo inaonesha kwamba utoaji wa fomu za kuwania uwakilishi pamoja na udiwani zitatolewa katika ofisi za Tume ya Uchaguzi zilizopo wilayani Unguja na Pemba.
Ratiba hiyo inaonesha kwamba kampeni za vyama vya siasa zitaanza rasmi Septemba 7, hadi siku ya mwisho kabla ya kuingia katika uchaguzi mkuu Oktoba 24 na kufuatiwa na upigaji kura. Katika taarifa hiyo imesema kwamba Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ipo katika hatua za mwisho za matayarisho ya upatikanaji wa vifaa vya kiutendaji katika uchaguzi.
Aidha hatua nyingine zilizotajwa ni pamoja na matayarisho ya kuweka hadharani daftari la kudumu la wapiga kura kwa ajili ya kazi za uhakiki wapiga kura ikiwemo kuweka pingamizi kwa watu ambao hawana sifa.
Upigaji kura katika uchaguzi mkuu utawahusisha wenye vitambulisho vya Mzanzibari mkazi kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ya Zanzibar ya mwaka 2006.
Jecha alisema mategemeo makubwa ya Tume ya Uchaguzi ni kuhakikisha kwamba uchaguzi unakuwa huru na kila taasisi na pande zinaheshimu matokeo hayo kwa mujibu wa sheria.
Aidha alizitaka asasi za kiraia pamoja na waangalizi wa ndani na nje wa uchaguzi mkuu kuheshimu sheria za uchaguzi kwa ajili ya kuepuka uvunjivu wa amani na utulivu.
Chama Cha Mapinduzi pamoja na CUF tayari zimekamilisha mchakato wa kutafuta na kupata majina ya wagombea nafasi za ubunge na uwakilishi Unguja na Pemba.

Imehaririwa na;- poatel Africa

Habari yako! Endelea kutembelea Tovuti ya TeknoTaarifa kwa Taarifa murwa za Teknolojia kutoka ndani na nje ya Tanzania, Tupo kwa ajili ya wapenzi wa Teknolojia.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post