Kampuni ya ubia ya UDART kwa kushirikiana na wakala wa mabasi yaendayo haraka (DART) inaanza leo kuendesha mafunzo kwa madereva kabla ya huduma ya usafiri kuanza rasmi Oktoba. Mabasi mawili yaliyoingizwa nchini ndiyo yatatumiwa katika mafunzo hayo.
Jana mabasi hayo yenye uwezo wa kubeba abiria wapatao 190 na jingine la abiria 100, yalipitishwa kwenye njia yake kuanzia Kivukoni hadi Ubungo na umma kutambulishwa juu ya mafunzo hayo leo.
“Kesho (leo) tunazindua mabasi mawili kwa mafunzo. Wakufunzi wametoka China...huduma kamili inaanza Oktoba,” Alisema Meneja wa Udart, Sabri Mabruk katika mkutano na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari. Ujio wa mabasi hayo na kuanza kwa huduma za BRT, kwa mujibu wa Mabruk, ndiyo mwisho wa daladala za kawaida kati ya Kimara na Kivukoni.
Alisema kutakuwa na utaratibu wa kulipa gharama za usumbufu kwa wenye mabasi na kisha kuwapangia njia nyingine.
Idadi ya mabasi yanayotarajiwa kutoa huduma chini ya mradi, ni 76.
Mabruk alisema mwezi ujao ndio watajua ni mabasi mangapi mengine yataletwa. Baada ya mafunzo ya wiki mbili kwa madereva, mabasi yaliyoko yatatoa huduma kupitia vituo 10 pekee kabla ya Septemba ambayo idadi ya mabasi itakuwa imekamilika.
Mabasi hayo yanayotarajiwa kutumia dakika 20 kutoka Kimara hadi Kivukoni eneo la Magogoni, ndani yana viti kwa ajili ya wazee, wajawazito na wenye ulemavu.
Pia yana mikanda maalumu ya kushika kwa abiria wanaosimama. Vile vile ilielezwa hayatakuwa na makondakta wala wapiga debe kutokana na mfumo wake wa kisasa wa ukusanyaji nauli.