Header ads

Header ads
» » Serikali imewataka wote Walionufaika na Mikopo HESLB wairejeshe

 
SERIKALI imewataka waajiri wote na wanafunzi walionufaika na mikopo ya elimu ya juu, kurejesha ili Watanzania wengine wanaohitaji wanufaike na mikopo hiyo. Aidha, imesema itaendelea kuiwezesha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kufanikisha shughuli zake ili wanafunzi wengi wapate mikopo.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa aliyasema hayo jana kwenye sherehe ya kuadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwa bodi hiyo pamoja na kuwakumbuka waanzilishi wake. Dk Kawambwa alisema waajiri wengi wamekuwa wakikaidi kuwalipia mikopo waajiriwa wao kitendo kinachokwamisha uendeshaji wa bodi hiyo.
Alisema endapo waajiri hao watalipa kwa wakati, wanafunzi wengine watapata fursa ya kunufaika mikopo hiyo ambayo itawasaidia katika masomo yao. “Ninawataka waajiri wote walionufaika na mikopo kurejesha ili wengine wanaohitaji waweze kunufaika na mikopo hiyo,” alisema.
Aliongeza kuwa serikali imeongeza bajeti ya bodi hiyo hadi kufikia Sh bilioni 341 mwaka huu kutoka Sh bilioni 56.1 mwaka 2005. Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya HESLB, Bertha Minja alisema kuwa mpaka sasa bodi hiyo imekusanya Sh bilioni 74.7 kwa mwaka wa fedha 2014/15 wakati 2005/2007 ilikusanya Sh bilioni 53.6 ya madeni yote.
Minja alisema tayari imekopesha Sh trilioni 2.09 kwa wanafunzi wa vyuo mbalimbali vilivyopo nchini. “Pamoja na mafanikio hayo, changamoto kubwa ni kutokubalika kwa sera ya uchangiaji ambapo wanafunzi wengi wanajua kuwa ni ruzuku, hivyo tunaendelea kuelimisha wanafunzi na umma kwa ujumla waelewe gharama za mikopo hiyo,” alisema Minja.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, George Nyatega alisema kuwa katika sherehe hiyo, wanawakumbuka waanzilishi wa bodi hiyo ambao ni aliyekuwa Waziri wa Sayansi , Teknolojia na Elimu ya juu, Pius Ng’wandu na aliyekuwa Waziri wa Elimu ya juu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Peter Msolla.
Alisema wanatambua mchango wa makatibu wakuu wawili wa wizara hizo akiwamo Dk Naomi Katunzi pamoja na wadau mbalimbali ambao kwa pamoja walishirikiana kuundwa kwa bodi hiyo.

Imehaririwa na;- poatel Africa

Habari yako! Endelea kutembelea Tovuti ya TeknoTaarifa kwa Taarifa murwa za Teknolojia kutoka ndani na nje ya Tanzania, Tupo kwa ajili ya wapenzi wa Teknolojia.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post