Kada wa CCM Ahmed Ismail aliyerusha risasi hewani katika ofisi za Chadema wilayani Bariadi amehukumiwa kwenda jela miezi sita au kulipa faini Sh2,000 baada ya kukutwa na hatia.
Ismail alikuwa akikabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya silaha.
Mwendesha Mashtaka, Yamiko Mlekano
alidai mahakamani hapo kuwa Aprili 22, mwaka huu, saa 10 jioni
mshtakiwa huyo alikwenda kwenye mkutano wa hadhara wa CCM katika Mtaa wa
Isanga akiwa na bastola.
Alidai
kuwa siku hiyohiyo, akiwa kwenye msafara wa Mbunge wa Bariadi
Magharibi, Andrew Chenge alitoa silaha hiyo hadharani kisha kufyatua
risasi tatu karibu na ofisi za Chadema wilayani humo kinyume cha
sheria.
Mshtakiwa alipotakiwa kujitetea kabla ya hukumu, aliomba Mahakama imuonee huruma kwa kuwa hakujua kama ilikuwa ni makosa.
Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Bariadi, Aidon Mwilapwa alitoa hukumu
hiyo baada ya kuridhishwa na ushahidi. Mshtakiwa huyo aliachiwa huru
baada ya kulipa faini.
Siku ya tukio Ismail alizua taharuki
baada ya kufyatua risasi tatu wakati msafara wa Chenge ulipokutana na
ule wa Chadema mjini Bariadi, Simiyu.