JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
TAREHE 8 MEI, 2015
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kukua kwa kasi kwa matumizi ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kumeleta mafanikio mengi katika
nyanja mbalimbali za maisha ya kila siku. Mafanikio haya yanathibitika kwa
kuongezeka kwa huduma za mawasiliano, huduma za kifedha na matumizi ya mitandao
ya kijamii. Aidha, mafanikio hayo yameleta changamoto nyingi katika
jamii. Changamoto hizo ni pamoja na kuibuka kwa makosa mapya ya jinai na
pia mbinu mpya za kutenda makosa ya zamani.
Ndugu Wananchi,
Makosa hayo hujumuisha uhalifu
wa Mitandao ambao simu za mkononi, kompyuta au mifumo ya kompyuta hutumika kama
nyenzo za kutenda uhalifu huo.
Mifano ya makosa hayo ni kama ifuatavyo:
1. Kumekuwepo na wizi wa fedha kwa
njia ya mtandao,
2. Kumekuwepo na ugaidi kupitia
kwenye mitandao,
4. Kuwepo na mmomonyoko mkubwa wa
maadili,
3. Kumekuwepo na uharibifu wa
miundombinu muhimu ya Taifa kwa makusudi, Kwa mfano kukatwa kwa makusudi Mkongo
wa Taifa wa Mawasiliano. [Hii imepelekea kuisababishia Serikali na Sekta
binafsi hasara na kusababisha kukosekana kwa huduma mbalimbali za kiuchumi na
za kijamii].
Ndugu Wananchi,
Kama mnavyofahamu kwenye kikao cha
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lililopita, Serikali ilipeleka Mswada
wa kutunga sheria ya uhalifu wa mtandao (Cyber Crimes) na Sheria hiyo
ilipitishwa na Bunge. Madhumuni ya kutunga sheria hii kama sheria nyingine
zilizotungwa na Bunge hapa nchini ni kutatua changamoto mbalimbali
zinazoikabili jamii hasa kwenye matumizi ya TEHAMA.
Ndugu Wananchi,
Ndugu Wandishi wa Habari,
Tanzania siyo nchi ya kwanza
kutunga sheria kama hii. Kuna nchi mbalimbali duniani zimetunga sheria
kama hii, kwa mfano nchi ya Uingereza (UK Computer Misuse Act, 1990), India (IT
Act, 2000), Malaysia (Computer Crime Act 2. ) Uganda (Computer Misuse Act,
2010), Korea ya Kusini (Information and Communications Network Act na Information
and Communication Infrastructure Protection Act), Singapore (The Computer
Misuse and Cybersecurity Act), Maturities (Computer Misuse and Cybercrime Act,
2003), Afrika ya Kusini, Marekani (Computer Fraud and Abuse Act, 1984)
na nyingi nyinginezo.
Ndugu Wananchi sasa mmepata pahala
pa kukimbilia, kwani mukitendewa uhalifu kupitia mitando sheria hii itawasaidia
kupata haki zenu. Ninawashangaa sana wale wanaopinga kutungwa kwa sheria hii
hapa Tanzania. Haikubaliki hata kidogo kuona Wantanzania wengine wanakumbana na
uhalifu kupitia Kwenye mtandao na wachache kwa faida zao binafsi wanataka
Serikali ikae kimya. Sheria hii haina tofauti na sheria za nchi nyingine nilizozitaja
hapo awali. Sheria hii imetungwa kwa mazingira ya nchi yetu ya Tanzania.
Ndugu Wananchi,
Sheria hii sasa
imeshasainiwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete baada ya kupitia hatua zote za kuiboresha. Hatua ya MWISHO
ilikuwa ni ile ya marekebisho yaliyofanywa na Bunge ambapo baadhi ya vifungu
vilivyolalamikiwa viliboreshwa. Kwa hivyo wananchi sasa tuipokee sheria
hii na kuitumia. Sheria hii ni nzuri na itasaidia sana kuwalinda wananchi,
mitandao na miundombinu yetu muhimu ya kitaifa.
Katika kuitumia sheria hii na kama
ilivyo kwa sheria nyingine yoyote, patakapoonekana kuna mapungufu, marekebisho
yatafanyika. Kwa hivyo kama kuna mtu yeyote mwenye maoni ya kuiboresha sheria
hii anaweza kuleta maoni Serikalini hapa Wizarani. Ninarejea tena: Waheshimiwa
Wabunge, Waheshimiwa Mabalozi, wadau mbalimbali wa Sekta ya Mawasiliano,
waandishi wa habari, wana-bloggers, na wananchi kwa ujumla kama kuna yeyote
mwenye maoni ya kuboresha kifungu chochote cha sheria hii alate maoni hayo hapa
Wizarani.
Serikali kupitia Wizara yangu
itapokea maoni au ushauri huo, tutayatafakari na kuyafanyia kazi kwa kina.
Haitosaidia sana kusema huko pembeni, jukwaa zuri la kuleta maoni ni kupitia
Wizara yangu.
Ndugu Wananchi, na
Ndugu Waandishi wa Habari,
Hii haitokuwa sheria ya kwanza
kufanyiwa marekebisho kama itaonekana kuna umuhimu wa kufanya hivyo.
Ahsanteni na
Ninawashukuru sana kwa kunisikiliza.