Wapinzani wamekusudia kuikwamisha Katiba Inayopendekezwa huku wakielekeza nguvu zao kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa lengo la kukiangusha chama tawala.
Mwaka huu una matukio makuu mawili ambayo
yanasubiriwa kwa hamu kubwa na Watanzania wengi ili kuandika historia;
upigaji kura wa kukubali au kuikataa Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi
Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.
Mambo hayo yanasababisha wanasiasa na vyama vyao
kuwa katika hekaheka kubwa ili kuhakikisha wanashinda katika matukio
hayo kulingana na msimamo wao.
Kumekuwapo na mgawanyiko katika suala la kuikubali
au kuikataa katiba hiyo na mvutano mkubwa upo kati ya Serikali kwa
maana chama tawala cha CCM na wapinzani chini ya muungano wao wa vyama
vitatu, Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi ambavyo vinaunda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa).
Silaha kubwa wanayoitumia Ukawa kwa sasa katika
kuikabili CCM ni kashfa ya ufisadi ya Akaunti Tegeta Escrow na msimamo
kwamba hawaiungi mkono Katiba Inayopendekezwa.
Kutokana na hali hiyo, CUF imefanya mkutano mkubwa
wa hadhara kwenye uwanja wa Mashujaa mkoani Mtwara ambako ilitumia
silaha hizo katika kushawishi wananchi kuiunga mkono.
Katika mkutano huo, mwenyekiti wa CUF, Profesa
Ibrahim Lipumba alimwalika mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), Zitto Kabwe ambaye kamati yake ndiyo ilishughulikia
sakata hilo kwa kutumia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG).
Ulikuwa ni mkutano uliopambwa na shangwe na
nderemo za kila aina kutoka kwa wafuasi wa CUF waliojitokeza kuwalaki
kwenye Daraja za Mikindani na kufanya maandamano ya zaidi ya magari 30,
pikipiki 300 na bajaji 40 na pikipiki huku wananchi wakiwa wamejipanga
kwenye mistari barabarani.
Baadhi walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali,
zikiwemo zilizokuwa na kibwagizo cha “tunataka fedha zetu za Escrow
zirudi... Mtumbwi wa Chenge umetoboka”. Andrew Change ndiye aliyekuwa
mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba.
Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mnyaa (CUF) alitumia
mkutano huo kuwaomba wananchi wa mkoa huo kupiga kura ya ‘hapana’ kwa
Katiba Inayopendekezwa wakati muda utakapofika.
Alisema Chenge na wabunge wenzake wa CCM
wametengeneza Katiba inayoendelea kulinda maslahi ya wachache badala ya
Watanzania wote.
“Ikiletwa hapa katiba ya Chenge ikataeni.
Ikataeni, tupeni kule kwani mkiikubali mtakuwa mnaungana na mafisadi
kuhalalisha vitendo vya kifisadi viendelee.