Kuanzia juzi, tumeona makala kwa njia ya picha kuhusu hali ya kutisha na kufadhaisha iliyopo katika Shule ya Msingi ya Nyamarere, Kata ya Ikome katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, mkoani Geita. Hakika ni picha ambazo zimewafanya baadhi ya wasomaji wetu kupigwa na butwaa kwa mshangao, huku wengine wakisema picha hizo ni za kusadikika, kwa maana ya kutoamini kwamba miaka 53 baada ya Uhuru bado kuna shule za ajabu ambazo hazina hadhi wala sifa ya kuitwa shule.
Ni picha zinazoonyesha hali halisi ya mazingira ya
kudhalilisha ya ufundishaji na ufundishwaji katika shule hiyo. Moja ya
maajabu ya shule hiyo ni kwamba inao wanafunzi 742 kuanzia darasa la
kwanza hadi la sita wanaotumia vyumba viwili tu vya madarasa, huku
wengine wakiwa nje wakisomea chini ya miti. Ajabu ni kwamba mahali ilipo
shule hiyo siyo mbali sana na anakoishi mbunge aliyechaguliwa na
wananchi pamoja na viongozi wa ngazi za kijiji, kata, wilaya na mkoa.
Viongozi hao hawajaguswa hata kidogo na matatizo yanayoikabili shule
hiyo ya Nyamarere.
Ni maajabu kwa kuwa walimu wanalazimika
kuwaelekeza wanafunzi kwa kuandika kwenye mchanga kutokana na madarasa
kutokuwa na mbao za kuandikia. Mwandishi wetu aliwakuta walimu
wakifundisha katika mazingira magumu ya kudhalilisha na kukatisha tamaa,
huku wanafunzi wakiwa wamekaa ardhini, wengine juu ya mawe na wengine
wakiwa wanachukua notisi huku wamechuchumaa. Shule hiyo haina madawati
na walimu hawana nyumba za kuishi.
Mmoja wa walimu alikutwa akifundisha wanafunzi wa
darasa la tatu namna ya kuumba herufi, lakini alikuwa akichora herufi
hizo hewani kutokana na kutokuwapo ubao. Mwingine alikuwa akifundisha
kwa imla kutokana na tatizo hilo, hivyo alilazimika kutamka na wanafunzi
kuandika, tena wakiwa wamekaa kwenye udongo. Mwalimu aliyekuwa
akifundisha hisabati darasa la pili hakuwa na ubao, hivyo kulazimika
kuandika juu ya mchanga. Majina na picha za walimu wote waliokutwa
katika mazingira hayo ya udhalilishaji yametokea gazetini sambamba na
wanafunzi waliokuwa wakiwafundisha.
Uamuzi wa kuchapisha picha nyingi badala ya makala
zenye maelezo marefu ulitokana na ukweli kwamba picha moja yaweza
kutuma ujumbe mzito zaidi kuliko makala ya maneno 1,000. Picha hizo
zinatoa ushuhuda usioacha shaka kwamba hiyo ndiyo hali halisi katika
shule hiyo. Lakini pia pengine zitatoa fursa kwa mamlaka hizo kuchukua
hatua stahiki, ingawa kuna ushahidi kwamba shule nyingi nchini
zinakabiliwa na mazingira magumu zaidi kuliko yaliyopo Nyamarere.
Hali hiyo inatia shaka kama kweli Mpango wa
Maendeleo ya Elimu ya Msingi nchini (MMEM), siyo kiini macho. Pamoja na
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kuweka vipaumbele tisa katika sekta
ya elimu, vipaumbele hivyo vimebakia tu katika makabrasha ya warasimu
serikalini. Serikali haijaonyesha dhamira ya kuimarisha elimu ya msingi.
Laiti ingetambua kwamba elimu ya sekondari au ya juu haiwezi kuimarika
pasipo kwanza kuimarisha ya msingi, ingewekeza hapo kwanza badala ya
kutumia rasilimali nyingi katika mipango mingine kama kujenga sekondari
za kata au kujenga maabara katika shule hizo kwa njia za zimamoto. Ni
kutokana na hali hiyo wanafunzi wanamaliza elimu ya msingi au ya
sekondari bila kujua kusoma wala kuandika.