Sheikh wa Msikiti wa Qiblatan,Sood Ally Sood (37) uliopo Kilombero jijini hapa amejeruhiwa kwa bomu la kurushwa kwa mkono alipokuwa akila daku nyumbani usiku wa kuamkia jana.
Pamoja na Sheikh Sood, mtu mwingine aliyekuwa
nyumbani kwake,aliyetajwa kwa jina la Muhaji Kifea (38) mkazi wa Sinza
jijini Dar es Salaam pia amejeruhiwa katika tukio hilo na wote wamelazwa
katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kwa matibabu.
Sheikh alijeruhiwa miguu yake yote na mapajani
huku Kifea akipata majeraha makubwa miguuni na kupoteza baadhi ya vidole
vya miguu yote.
Akizungumza hospitalini hapo, Sheikh, Sood alisema
tukio hilo lilitokea nyumbani kwake eneo la Majengo ya chini, usiku wa
kuamkia jana saa 5:00 wakati yeye pamoja na mgeni wake walikuwa wakila
chakula sebuleni.
“Nikiwa sijui hili wala lile nilishtushwa na
mlipuko ulioambatana na vyuma mbalimbali vilivyokuwa vikiruka hewani
ambapo bomu hilo linaelezwa kuwa ni guruneti lililorushwa kupitia
dirishani baada ya watu wasiofahamika kufanikiwa kuvunja kioo cha
dirisha la chumba tulichokuwamo,” alisema Sheikh Sood.
Alidai anawajua waliotekeleza shambulio hilo kwa
sababu amekuwa akipokea vitisho kutoka kwa watu anaowafahamu na tayari
alikuwa ametoa taarifa kwa vyombo vya dola.
Alisema kuwa siku tatu kabla ya tukio hilo
alikoswakoswa kupigwa risasi na watu wasiofahamika wakati akitoka
msikitini na akatoa taarifa Kituo Kikuu cha Polisi jijini Arusha kuhusu
tukio hilo. Sood anasema kuna baadhi ya vijana anawatuhumu juu ya
matukio hayo.
Sheikh huyo ambaye ni Kiongozi wa dhehebu la
Answar sun Kanda ya Kaskazini amekuwa akitofautiana na waumini wenzake
kutokana na msimamo wake wa kutokukubaliana na baadhi ya waumini wenye
msimamo mkali wa msikiti huo.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo alikemea
matukio ya mabomu yanayolitikisa Jiji la Arusha katika siku za karibuni
na kuviagiza vyombo dola kufanya uchunguzi wa kina kubaini wahusika wote
ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
“Uchunguzi wa awali unaonyesha tukio hili
limetekelezwa na watu walio karibu na Sheikh. Polisi wanaendelea na
uchunguzi kwa sababu baadhi ya watu wanaotajwa kuhusika kwenye tukio
hili pia ni miongoni mwa watuhumiwa kwenye matukio mengine ya milipuko
ya bomu Arusha,” alisema Mulongo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatusi
Sabasi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa majeruhi
wanaendelea vyema huku polisi wakiendelea na uchunguzi wa kina kuwabaini
wahusika.
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alielezea
kusikitishwa na matukio ya milipuko ya mabomu Arusha na kuliomba jeshi
la polisi kufanya uchunguzi wa kina kuwakamata wahusika bila kujali
vyeo, nyadhifa, dini, itikadi wala rangi zao.