Majaribio ya chanjo mpya ya malaria ijulikanayo kama PfPZ ambayo mtu akipatiwa hataugua tena ugonjwa wa malaria maisha yake yote, yataanza kutolewa nchini mwezi ujao.
Aidha, matayarisho kwa ajili ya kazi hiyo yameshakamilika na watu 54, wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35, wameshaandikishwa kwa ajili ya kufanyiwa utafiti huo.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Afya Ifakara (IHI), Dk. Salim Abdullah, aliyasema hayo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari mwishoni mwa wiki iliyopita.
Alisema Tanzania ni nchi ya kwanza barani Afrika kunufaika na majaribio ya chanjo iliyotengenezwa na kampuni ya Sanaria ya Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, majaribio hayo yatafanyika katika Taasisi ya Afya ya Ifakara kwenye hospitali yake ya tiba iliyoko Kingani, wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.
Matokeo ya majaribio ya mwanzo ya chanjo hiyo yaliyofanyika nchini Marekani kuonyesha kuwa inatoa kinga kwa asilimia 100 dhidi ya kimelea cha malaria cha Plasmodium falciparum, ambacho husababisha vifo vya zaidi ya watu 600,000 kwa mwaka.
“Tunataka kuona kama matokeo hayo yaliyoonekana Marekani yanaweza pia kuwa hivyo hapa Afrika, tunahitaji kuone ikiwa tunaweza kuboresha matokeo hayo kwa kuongeza kiasi cha chanjo (dose), badala ya kufanya ufuatiliaji kwa miezi mitatu kama walivyofanya kule Marekani, sisi tutafuatilia utendaji kazi wa chanjo hii kwa mwaka mzima,” alieleza.
IHI ambayo ni moja ya taasisi zinazoongoza katika utafiti wa magonjwa hasa malaria barani Afrika pia imeshiriki kwenye majaribio ya kinga nyingine ya malaria ijulikanayo kama RTS,S ambayo pia imeonyesha mafanikio ila inaendelea kufanyiwa utafiti.
Ukiacha faida kwa watu wa kawaida barani Afrika na maeneo mengine duniani yanayoathirika na malaria, chanjo inawalenga pia watalii, wanadiplomasia, wafanyabiashara wanaosafiri, wafanyakazi wa huduma za misaada na wanajeshi katika kujikinga na malaria.
Chanjo hiyo inafanyika nchini wiki kadhaa baada ya wanasayansi wa Marekani kutangaza kugundua chanjo hiyo ambayo mtu akipatiwa hataugua tena ugonjwa wa malaria maisha yake yote.
Taarifa ya Taasisi ya Marekani ya Kudhibiti Magonjwa ya Kuambukiza na Mzio (NIAID), iliyotolewa mwanzoni mwa mwezi huu, ilieleza kuwa ugunduzi huo ambao tayari umefanyiwa majaribio kwa watu kadhaa, umeonyesha mafanikio kwa asilimia 100 na kwamba utaandika historia ya kufuta malaria na kuwa ugonjwa wa nadra kwa watu kuugua.