Wakati CCM ikifanya jitihada za kudhibiti makada wake wanaotajwa kuwania urais, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal amemtuma waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuendesha moja ya shughuli ambazo chama hicho kinaamini kuwa ni moja ya majukwaa ya kampeni kwa wagombea.
Dk Bilal amemtuma Lowassa, mmoja wa makada
wanaotajwa kutaka urais, kuongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa
msikiti wa Patandi mkoani Arusha Alhamisi wiki hii, ambako habari
zinasema siku mbili baadaye huenda mbunge huyo wa Monduli akatangaza
rasmi nia yake ya kuanza safari ya kuelekea Ikulu kwa tiketi ya CCM.
Taarifa iliyotolewa jana na mwandishi wa habari wa
Makamu wa Rais, Boniface Makene inaeleza kuwa Dk Bilal anakabiliwa na
majukumu mengine ya kitaifa na hivyo ametoa ombi maalumu la kuwakilishwa
kwenye harambee ya kukamilisha ujenzi wa msikiti huo ulioanza mwishoni
mwa miaka 90.
“Makamu wa Rais ameona kuwa shughuli hii ya
uchangiaji wa ujenzi wa msikiti isisogezwe mbele kumsubiri, bali
iendelee kwa kuwa anaamini Lowasa ana uzoefu katika kufaninikisha
shughuli za aina hii. Pia mchango wake katika shughuli za harambee
katika shughuli ni wa mfano,” inasema taarifa hiyo.
Pia taarifa hiyo ilieleza kuwa mchango wa
wanajamii wanaoswali katika msikiti wa Patandi ni mkubwa kwani wamekuwa
wakijitoa kwa namna nyingi kujenga mshikamano baina ya jamii
zinazowazunguka bila kuwa na vikwazo na wameshiriki kuwasaidia watoto
yatima.
Uamuzi huo wa Dk Bilal, ambaye kwa nafasi yake
anaingia kwenye vikao vyote vya juu vya chama tawala, vikiwamo vya
Zanzibar, utakuwa umetikisa harakati za kudhibiti baadhi ya makada
wanaotajwa kuwania urais, hasa kambi ya Lowassa ambayo inasemekana
inalalamikia kuchezewa rafu na uongozi wa CCM, ingawa haijabainisha rafu
hizo.
Lowassa ni mmoja wa makada sita waliopewa onyo
kali na CCM Februari mwaka jana, likiwazuia kujihusisha na uchaguzi kwa
zaidi ya miezi 12 baada ya kubainika kuwa walianza kampeni mapema kwa
kushiriki vitendo vinavyokiuka maadili, zikiwamo za harambee na hivyo
kutakiwa kuomba kibali kabla ya kushiriki.
Hata hivyo, wiki mbili zilizopita Lowassa na
makada wengine wanaotajwa kuwania urais walialikwa Zanzibar kwenye
harambee ya kuchangia mfuko wa maendeleo wa mkoa mpya wa Magharibi,
ikiwa ni mara ya kwanza kushiriki tangu walipofungiwa na chama hicho
mwaka jana.
Wasomi waliotafutwa na Mwananchi kuzungumzia uteuzi huo walikuwa na maoni tofauti.
“Sina mengi, hakuna atakayeshindwa kuona kuwa wana
mu-endorse (wanamuunga mkono) huyo. Yeye (Lowassa) ni miongoni mwa watu
wanaotajwa kuwania urais, kwa hiyo hii ni moja ya ‘technic’ mbinu,”
alisema Profesa Tolly Mbwete ambaye ni mkuu wa Chuo Kikuu Huria.
Alisema uteuzi huo ni miongoni mwa harakati za kumuweka vizuri Lowassa katika uchaguzi ujao.
Lakini mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema iwapo Lowassa amepewa
jukumu hilo na Dk Bilal, maana yake ameonekana ana uzoefu na anaifahamu
kazi hiyo na aangaliwe kama waziri mkuu mstaafu na si vinginevyo.