UPASUAJI wa kutenganisha watoto wawili waliozaliwa wameungana viunoni, unatarajiwa kufanyika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam. Katika upasuaji huo ambao mara ya mwisho ulifanyika 1980 chini ya Profesa Shija, madaktari bingwa saba wanatarajiwa kutenganisha watoto hao waliozaliwa Zanzibar.
Katika upasuaji huo wa 1980, watoto waliotenganishwa walizaliwa wakiwa wameungana tumboni. Hata hivyo, haikuelezwa zaidi kama walipona au la.
Mmoja wa madaktari hao, Dk Zaituni Bohari, akizungumza na gazeti hili jana, alisema hadi kesho wakati wa upasuaji huo watoto hao watakuwa wamefikisha umri wa siku 23.
Dk Bohari alisema watoto hao, wamepungukiwa na viungo ambapo mmoja amepungukiwa zaidi-lakini hakutaka kuvitaja-kuliko mwingine ambaye hana sehemu ya haja kubwa.
Alisema hospitali hiyo ilipokea watoto hao wakiwa na siku nne kutoka visiwani humo na madaktari hao wamejiandaa kushiriki upasuaji huo kwa umakini mkubwa. Akifafanua, daktari huyo alisema hajui upasuaji huo utachukua muda gani kwa sababu unahusu masuala mengi ya kuzingatia na unahitaji utulivu wa akili.
Hofu ya mmoja Alieleza wasiwasi wake kuhusu uwekezano wa mtoto aliyepungukiwa viungo vingi kupona na kufafanua, kwamba ikibidi watajitahidi kuokoa mmoja ambaye anaonesha matumaini ya kuishi.
“Katika upasuaji huo, tutajitahidi mmoja apone na lengo likiwa ni kuokoa mwenye viungo vilivyokamilika na kumfanyia upasuaji mwingine wa kumtengenezea sehemu ya muda ya kutolea haja kubwa.
“Kwa sasa anatumia sehemu ya uke kujisaidia, jambo linaloweza kumsababishia magonjwa ya maambukizi kutokana na kupitisha uchafu huo mahali pasipotakiwa,” alisema Dk Bohari na kusisitiza kuwa madaktari bingwa wanaoaminika, watashirikiana kufanya upasuaji huo kwa karibu ili kuokoa maisha.
Akieleza historia ya watoto hao, Dk Bohari alisema walizaliwa Agosti 7 lakini hakutaja majina ya wazazi wao.
BAHTISMA BLOG CHAGUO LA WATU