Header ads

Header ads
» » Serikali kutoa bilioni 2.5/- kwa ajili ya Taasisi ya Moyo

 
SERIKALI itakuwa inaokoa Sh bilioni 2.5 kwa mwaka baada ya kuzindua Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, ambayo ni ya kisasa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Fedha hizo zilikuwa zikitumika kwa ajili ya kuwasafirisha Watanzania na kwenda kutibiwa magonjwa ya moyo katika hospitali mbalimbali nje ya nchi.
Lakini, sasa tiba ya magonjwa ya moyo itakuwa ikipatikana hapa nchini katika taasisi hiyo, iliyopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam. Akizungumza kwenye uzinduzi huo jana, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alisema taasisi hiyo imeanzishwa kwa msaada wa serikali ya China, ambayo ilitoa Sh bilioni 16.6 zilizotumika kujenga jengo hilo la kisasa la moyo.
“Jitihada za kupatikana msaada huo wa fedha zilifanywa na Rais Jakaya Kikwete alipotembelea China na kukutana na Rais Hu Jintao wa China, hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi pekee yenye taasisi ya moyo ya kisasa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati,” alisema Dk Rashid.
Dk Rashid aliyekuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Kikwete, alisema taasisi hiyo tayari imehudumia wagonjwa 14,000 ambapo 912 kati yao walilazwa na 148 walifanyiwa upasuaji wa moyo na kupona. “Taasisi hii ina vifaa vya kisasa vilivyoigharimu serikali shilingi bilioni 10 kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wanapata matibabu ya moyo nchini mwao badala ya kuingia gharama zaidi kwenda nje ya nchi,” alisema Waziri huyo.
Dk Rashid alisema ugonjwa wa moyo ni wa pili kwa kusababisha vifo vingi nchini, baada ya magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi na ndio maana Rais Kikwete alilitambua hilo na kuweka jitihada nyingi, kuhakikisha ugonjwa huo hauendelei kuwasumbua Watanzania.
Alisema serikali imetoa maagizo kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kugharimia matibabu ya wanachama wa mfuko huo wenye matatizo ya moyo hapa nchini ili taasisi hiyo ihudumie Watanzania wengi zaidi.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Donan Mbando, alisema mpaka kufikia Julai mwaka huu wagonjwa 45 walifanyiwa upasuaji kwenye taasisi hiyo na kupona, huku 200 wakifanyiwa uchunguzi wa mishipa ya moyo kwa kutumia mashine za kisasa zilizoko kituoni hapo.
Alisema tayari Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imeamua taasisi hiyo ihudumie watoto wenye matatizo ya moyo kutoka nchi zote za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na itakuwa ikiwalipia watoto 60 gharama za matibabu kila mwaka.
Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Muhimbili, Profesa Joseph Kuzilwa alisema Muhimbili inajivunia mafanikio ya kuwa na taasisi hiyo, ambayo wameipa jina la Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI) kama ukumbusho na kuthamini juhudi za Rais Kikwete za kuhakikisha taasisi hiyo inapatikana hapa nchini kusaidia wananchi.

Imehaririwa na;- poatel Africa

Habari yako! Endelea kutembelea Tovuti ya TeknoTaarifa kwa Taarifa murwa za Teknolojia kutoka ndani na nje ya Tanzania, Tupo kwa ajili ya wapenzi wa Teknolojia.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post