Chama cha Wafanyakazi Madereva Tanzania (Tadwu) kimeazimia kufanya mgomo nchi nzima Agosti 17, mwaka huu ambao pia utahusisha daladala endapo madai yao hayatafikiwa katika kikao kitakachofanyika Alhamisi wiki hii.
Kikao hicho cha
kamati maalumu iliyoundwa na Waziri Mkuu ili kujadili matatizo katika
sekta ya usafirishaji, kitajadili mikataba, posho, mishahara na
mazingira ya kazi kwa madereva wa Tanzania.
Akizungumza
Dar es Salaam jana katika mkutano uliowakutanisha madereva 1,400,
mwenyekiti wa Tadwu, Shaaban Mdemu alisema wamechoshwa na utendaji kazi
wa kamati hiyo kwa sababu inapeleka ajenda nyingine bila kujadili
masilahi ya madereva.
Mdemu alisema mkutano ujao
utakuwa ni wa mwisho kuhudhuria na matokeo ya kikao hicho ndiyo
yatakayoamua kama watafanya mgomo au la.
Alisema madai yao yalitakiwa kumalizwa ndani ya siku saba baada ya kuundwa kwa kamati hiyo, lakini sasa ni mwezi wa tatu.
“Tunachotaka
madai yetu yatekelezwe. Bila maafikiano hatutaelewana na Jumatatu ijayo
hakuna dereva yeyote atakayeingiza gari barabarani,” alisema kiongozi
huyo na kuungwa mkono na madereva waliohudhuria mkutano huo.
Mdemu
aliwalaumu pia wamiliki wa vituo vya mafuta kwa kuwakata fedha zaidi
kwa kila lita ya mafuta kwa madai kuwa wanasababisha hasara kwa kiasi
kinachobainika kupungua wanapofikisha mzigo sehemu husika.
“Wamiliki
wa vituo vya mafuta wanatukata Sh5,000 kwa kila lita ya mafuta
yanayopungua, hili nalo tutalifikisha kwenye kamati ili lijadiliwe na
kutafutiwa ufumbuzi,” alisema.
Naibu Katibu Mkuu wa
Tadwu, Rashid Saleh aliwataka Watanzania wajue kuwa uamuzi wao wa
kusitisha huduma unatokana na Serikali kutokuwa na dhamira ya dhati ya
kutatua malalamiko ya madereva ambayo ni ya muda mrefu sasa.
Alisema madereva wa Tanzania hawafanani na wengine wa nchi jirani kwa sababu wana hali mbaya kimasilahi.
“Siyo
lazima kila mtu anunue lori, tunataka kampuni chache zenye magari mengi
na zinazolipa madereva vizuri. Hawa matajiri wenye magari mawili ndiyo
wanaotusumbua kwenye masilahi,” alisema Saleh.