Header ads

Header ads
» » UKAWA nao kumtangaza mgombea wao Jumanne ijayo.


Mvutano mkali ulioibuka jana katika kikao cha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumchagua mgombea urais atakayeviwakilisha katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, umesababisha kushindwa kumtaja mgombea wake wa urais.
Kutokana na mvutano huo, viongozi wa vyama hivyo waliahirisha kikao hicho na kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa watamtangaza mgombea huyo Jumanne ijayo.
Kikao hicho kilichowahusisha wabunge wote na viongozi wakuu wa vyama vya Chadema, NLD, CUF na NCCR-Mageuzi vinavyounda Ukawa, kilifanyika jana katika ukumbi wa Millenium, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alishindwa kuwaeleza wanahabari kilichowakwamisha kumtangaza mgombea, huku akisisitiza kuwa wanataka kuweka mambo sawa.
“Hatuwezi kuwaangusha Watanzania na kipindi hiki ndiyo chetu kwani tunaingia katika uongozi wa Serikali ili kulikomboa taifa,” alisema: “Kuna mambo ya kukubaliana na kuweka sawa, tutamtaja mgombea wetu Julai 14 (keshokutwa). Naomba niwaeleze Watanzania kuwa Ukawa haiwezi kuvunjika tunachokifanya ni kuwa makini katika maamuzi yetu.”
Alisema kikao cha Kamati ya Ukawa kilifikia muafaka na jana kuwasilisha mrejesho kwa wabunge ndipo ulipofikiwa muafaka wa kusubiri hadi keshokutwa, huku akisisitiza kuwa katika kugawana majimbo wamekubaliana kwa asilimia zaidi ya 90.
Alipobanwa aleleze ni mambo gani yaliyokwamisha kufikiwa kwa muafaka alisema: “Kuna mambo ya kujadiliana baina ya vyama vyetu ila hayawezi kuleta matatizo, tupo pamoja na tutatoa jibu la pamoja.”
Alisema Ukawa imetokana na maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya, hivyo kiongozi atakayepitishwa na chama hicho lazima awe, mwadilifu, muwazi na mwajibikaji.
“Lazima tuwe na mgombea atakayesimamia mambo ya wananchi waliyotaka yawemo katika Katiba, mambo hayo ni yale yaliyowekwa katika rasimu ya Katiba ya Jaji (Joseph) Warioba,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema kama katiba ya nchi ingekuwa na kifungu kinachoruhusu vyama kuungana, vyama vinavyounda Ukawa vingeungana lakini kutokana na sintofahamu hiyo katika Katiba, wanalazimika kutatua changamoto hiyo kwa umakini mkubwa.
Kuhusu majimbo alisema; “ni kama tumeshagawana yote isipokuwa ambayo yana wagombea wawili wawili, yaani kutoka vyama zaidi ya viwili. Tumekubaliana majimbo zaidi ya 170 mpaka sasa.”

Imehaririwa na;- poatel Africa

Habari yako! Endelea kutembelea Tovuti ya TeknoTaarifa kwa Taarifa murwa za Teknolojia kutoka ndani na nje ya Tanzania, Tupo kwa ajili ya wapenzi wa Teknolojia.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post