Kati ya hizo, tayari Sh milioni 30 zimeshatumika kwa kumuongezea mkataba kiungo wake, Said Ndemla, hivyo sasa zimebaki Sh milioni 170.Simba ilipanga pia kumpa mkataba mpya winga wake, Ramadhan Singano kwa dau la Sh milioni 30 lakini mwenyewe amezikataa akitaka apewe Sh milioni 50 taslimu.
Mmoja wa watu muhimu katika Kamati ya Utendaji ya Simba na Kamati ya Usajili, amesema kiasi hicho cha fedha kitatumika kwa ajili ya kusajili wachezaji makini watatu hadi wanne ili kuimarisha kikosi chao msimu ujao.Chanzo hicho kilisema, kati ya wachezaji hao wamepanga kusajili mshambuliaji mmoja kutoka Burundi na wengine wazawa waliowaona kwenye usajili wa msimu huu.
“Katika msimu huu hatutaki kutumia fedha nyingi za usajili, tumeona hakuna haja kwa sababu timu haishiriki michuano migumu ya kimataifa. “Tumetenga Sh milioni 200 kwa ajili ya kusajili wachezaji kati ya watatu hadi wanne tutakaowatumia kwa ajili ya msimu ujao wa ligi,” kilisema chanzo hicho.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hans Poppe, ameliambia Championi Jumamosi: “Tutasajili wachezaji watatu tu wenye uwezo, hatutasajili wachezaji wengi kwa ajili ya msimu ujao. Kati ya wachezaji tutakaowasajili, mmoja atakuwa ni mshambuliaji wa kigeni.”